Makala

KINAYA: ‘Ouru’ hapaswi kuvuruga vita vya ‘Baba’ na Samoei, ni kadhia safi

March 1st, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

‘OURU’ asitucheze shere! Naam, ukimwona mwambie hivyo.

Hatutaki mchezo wa paka na panya. Kumbuka mjinga akierevuka, mwerevu yu mashakani.

Nimesikia fununu zinazonasibishwa na yule ‘Malkia’ wa Kirinyaga aliyetuhumiwa kuchovya buyu la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) zikanishtua.

Zinasema vipi kwani? Eti ‘Ouru’ ni mcheza-kamari mjanja anayeficha kadi fulani vizuri ili akiiangusaha saa zake amalize kamari mara moja, kwetu kuende kilio, kwake kicheko.

Eti mpango wa maridhiano (BBI) unakusudiwa kuunda vyeo kadhaa ili ‘Ouru’ amrithishe anayemtaka, ‘ufalme’ usiwahi kutoka karibu na mlimani. Ajabu!

Si kwamba najali hata! Nimetawaliwa na wa milimani, nikatawaliwa na mwendazake Mzee Kirungu, Mungu akaniweka hai, na maisha yanaendelea vyema tu mpaka sasa.

Mwamuzi wa mwisho ni Mungu. Hata nikiamka nisikie Mungu ameamuru tukae bila kiongozi walivyokuwa Wana wa Israeli kabla ya kuingia ujanja, nitaridhia tu. Simpingi.

Lakini tukubaliane hapa: ‘Ouru’ si Mungu, hivyo lolote analosema nina haki ya kulipinga na kueleweka nilivyo.

Naam, kama hilo la kuwa kinara wa nchi na pia ‘gavana’ mwenza wa Nairobi. Kituko hicho hasa! Wakenya mnachekesha kweli! Au, bora zaidi, mnahuzunisha hasa!

Ulikwenda wapi ule ukali wenu wa jadi wa kutetea haki zenu? Ujasiri mlipeleka wapi? Au mlihasiwa na nani? Jongoo hapandi mtungi tena?

Sasa utazoea kuniamini nikikwambia jamaa ana uchu wa mamlaka, labda haendi popote baada ya 2022. Kwangu si neno, awepo asiwepo yote mamoja.

Hata hivyo, bado ninamwomba asitucheze shere. Asivuruge kinyang’anyiro cha 2022 ambacho kinaendelea kuchukua mkondo wa kupendeza sana.

Ikiwa una akili timamu, hata robo ya zangu, nina hakika unajua kuna uwezekano mkubwa kwa ‘Baba’ kuzichapa na Dkt Bill Samoei ifikapo 2022.

Hicho kitakuwa kinyang’anyiro cha kupendeza. Ni kama kutazama mechi ya kabumbu kati ya Arsenal na Manchester United.

‘Baba’ na Daktari wameliliana maini kwa zaidi ya miaka 10. Hebu na wachaniane magwanda bila kusumbuliwa na mtu wa tatu.

Mtu wa tatu hapa ni huyo anayeitwa kadi ya siri ‘Ouru’. Asivuruge mambo. Sina soni wala uoga nikisema kutia kura kwenye debe ambamo mwaniaji wa mlimani yupo!

Kisa na maana? Inatabirika. Wingi wa siafu unaathiri matokeo na kuyafanya ya kutabirika upesi, hasa wakiamua kurauka alfajiri kwenda kutetea ‘ufalme’.

Kwa kutaka kushuhudia kinyang’anyiro cha kweli ambapo kina mwana wa mlimani hawana maslahi ya moja kwa moja, namwomba ‘Ouru’ awe mzalendo wa kweli.

Mzalendo wa kweli kivipi? Awaachie ‘Baba’ na Dkt Bill wamenyane kama dume. Hicho ni kinyang’anyiro ambacho kitapendeza sana.

Kitatuonyesha tabia za siafu wa mlimani katika hali ambapo hawana ‘sungari nguru’ wanayoendea Ikulu, tuone iwapo watarauka kumpigia ‘mtu mwingine’ kura.

Vilevile, kitapendeza kikweli kwani kitakuwa kati ya mwalimu na mwanafunzi.

‘Baba’ amedai ndiye mwalimu wa kisiasa wa Dkt Bill, japo mzaliwa wa Sugoi kawa sugu kweli!

Tutakapoanza kuwachagua watu kutokana na utendakazi na tajiriba yao badala ya msukumo wa kikabila tutakuwa tumekomaa kiakili. Akili si kofia, zitumie vizuri.

 

[email protected]