Makala

KINAYA: Punguza Mizigo, Kujenga Daraja hazina tofauti, wembe ni ule ule

July 28th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

KAA kando ujionee ukichezwa shere sasa!

Hapa wa kutapeliwa ni wewe, si hao unaoita waheshimiwa ila unawachukia hadi ya kuwachukia.

Hiyo unayoshabikia eti ni fursa yako kujinusuru, ukiiita kwa bashasha eti ‘Punguza Mizigo’, ni janja ya kukupumbaza ili ujipate mtegoni ndani, usiweze kujinasua.

Hebu subiri kidogo… Nusura busara za kikamba zinipotoshe. Wazee wangu wakinikumbusha mara kwa mara kwamba uswahili (ujanja) wa nyani huishia jangwani!

Kisa na mkasa? Huko hakuna miti ya nyani kupanda, kuruka kutoka mti mmoja hadi mwingine wala kuning’inia matawini akikwepa hatari na kumdhihaki anayemkimbiza.

Nilidhani uswahili wa wanasiasa umewafikisha jangwani, wakakosa angaa mti wa kujishikilia, kumbe nilinoa kishenzi!

Nilidhani wajanja watatu wakuu zaidi nchini – ‘Ouru’, Dkt Samoei na ‘Baba’ – wangeangamizwa kisiasa na mpango wa ‘Punguza Mizigo’. Niliamini mpango wao mbadala wa kubadili Katiba kupitia lile jopo la upatanisho waliitalo ‘Kujenga Madaraja’ ungekwama mara moja kwani wametanguliwa na ‘Punguza Mizigo’.

Nusura nianze kushangilia kwa kujishasha-shasha nikidhani wajanja hao waliotudhibiti kisiasa miaka yote hii wamepatikana.

Kumbe nilinoa! Mpaka sasa naamini wajanja hao walisaidia kwa mbali harakati za kukusanya sahihi ambazo ziliwezesha kuidhinishwa kwa mpango wa ‘Punguza Mizigo’.

Hata ikiwa si wote, labda wawili kama ‘Ouru’ na ‘Baba’ hivi, kwani walijua ripoti ya jopo lao la ‘Kujenga Madaraja’ iko njiani.

Naamini walitaka mipango yote miwili ikinzane, Wakenya tuzugike akili na kuamini kwamba masaibu ya nchi hii hayaishi bila kura ya maamuzi.

Kisha? Tukubali mipango yote miwili – ‘Punguza Mizigo’ na ‘Kujenga Madaraja’ – ioanishwe kisha tupate pendekezo moja la kupigia kura ya maamuzi.

Kwa nini tusilipigie kura pendekezo la kwanza, ‘Punguza Mizigo’, ambalo tayari limepokelewa na kukubaliwa rasmi na ile tume ya kifumba-macho, almaarufu IEBC?

Pendekezo la ‘Punguza Mizigo’, hata kwa mtu asiye na akili, haliwezi kupitishwa na bunge! Baadhi ya mambo ambayo linapendekeza ni kuwafuta kazi wabunge wengi.

Kivipi? Kwa kupunguza maeneo bunge, kuondolea mbali viti vya wanawake wanaowakilisha kaunti, kaunti zenyewe zipunguzwe, yaani mambo ya ajabu tu!

Hata wewe, ikiwa una akili razini, utakubali kitu ambacho kitakufuta kazi? Si huko ni kujitia kitanzi kwa kweli?

Utakuwa una haja gani kuishi huku duniani ikiwa hata maslahi yako mwenyewe huwezi kuchunga? Utayachunga ya nani ikiwa yako yanakushinda?

Hilo, nakuapia Jalali, halijatokea kibahati mbaya. La hasha! Limepangwa hivyo ili kwanza limshtue mbunge wako, kisha likushtue wewe ukisikia ene-bunge lako litafutwa!

Kisha? Wewe na mbunge wako mseme hamtaki mapendekezo hayo, eti heri mwangalie yale ya ‘Kujenga Madaraja’ yakoje.

Kufumba na kufumbua, wajanja watatu ‘Ouru’, Dkt Samoei na ‘Baba’ wapendekeze tuunganishe mapendekezo yote mawili halafu tuyapigie kura ya maamuzi.

Acha kulalia masikio kabwela mwenzangu, janjaruka! Tunatapeliwa kama washamba waliofika Nairobi leo asubuhi kutoka mashambani. Tusikubali.

Tusipige kura ya maamuzi kubadili Katiba isiyotudhuru kwa vyovyote kina yakhe.

Viongozi wanataka vyeo na pesa zaidi, sisi hawatuahidi chochote.

Wallahi tusitoke bure.

 

[email protected]