Habari Mseto

Kinaya Ruth Odinga akisifia utawala Gavana wa UDA

March 4th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Kisumu, Ruth Odinga, amemsifu Gavana wa Kwale, Fatuma Achani, kwa uongozi wake.

Bi Odinga ambaye ni dadake kinara wa ODM, Raila Odinga, alisema gavana huyo aliyechaguliwa kwa tikiti ya Chama cha UDA ameweza kuwapa kina mama zabuni katika miradi ya serikali ya kaunti.

Akiongea kwenye hafla ya wanawake katika Wadi za Waa, Ng’ombeni na Ramisi, aliwataka kina mama kumuunga mkono Bi Achani akimtaja kuwa kielelezo bora kwa wanawake.

“Hii inapiga jeki kina mama na wanahamasishwa kuhusu biashara mbalimbali zilizoko katika serikali ya kaunti. Hii ni hatua bora na muhimu sana,” alisema Bi Odinga.

Bi Odinga alisema wakati umefika wanawake kutobaguana kwa misingi ya vyama vya kisiasa bali washirikiane kimaendeleo.

“Msiangalie chama, angalieni kiongozi. Kama ni mwanamke mwenzetu hebu tumpigie debe na kumuunga mkono. Mwanamke akifanikiwa, jamii nzima hasa kina mama wengine walioko chini wanainuliwa,” akasema.

Tangu aingie mamlakani miezi 17 iliyopita Bi Achani amekuwa akiwashawishi kina mama kubuni kampuni ili wapate zabuni zinazotolewa katika serikali ya kaunti.

Mvurei Women Company Limited ni mojawapo ya kampuni ambazo zilipewa zabuni ya Sh3 milioni.

Bi Odinga, aliwasihi kina mama hao pia kuanzisha mpango wa kukusanya fedha kwa makundi almaarufu ‘Table Banking’ ili kuwasaidia zaidi kufanya biashara na serikali ya kaunti.

Mbunge huyo wa kike alisema Bi Achani, ambaye miaka 10 iliyopita alikuwa Naibu Gavana wa Kwale, ni rafiki yake.

“Alikuwa naibu gavana wakati nilipokuwa nikishikilia nafasi sawa na hiyo. Najua hatuko kwenye chama kimoja lakini kazi yake inaonekana. Bi Achani anafanya kazi nzuri sana,” alisema Bi Odinga.

Alikuwa ameandamana na Mbunge wa Malindi, Bi Amina Mnyazi, ambaye pia ni mwanachama wa ODM.

Bi Mnyazi alisema Bi Achani ameweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza aliyeshinda ugavana eneo la Pwani na kufikia sasa anaendelea kuonyesha mfano bora wa kuigwa.

“Wanawake wa Kwale ni wa nguvu tukianza na mwakilishi wa wanawake, Fatuma Masito halafu Gavana Achani. Ijapokuwa hatuko chama kimoja, tunamtambua Gavana Achani,” Bi Mnyazi akasema.

Sifa za wawili hao kwa Bi Achani zinatolewa miezi michache baada ya Bw Odinga kuzuru kaunti hiyo na kuacha bughudha kwa viongozi wanaoegemea upande wa Bi Achani ambao walidai alimdhalilisha kwenye hotuba zake.

Miongoni mwa waliokosoa matamshi ya Bw Odinga dhidi ya Bi Achani ni Waziri wa Jinsia, Aisha Jumwa.

Kwa upande wake, Bi Masito aliwasihi wanawake wa Kwale kuchagua mwanamke kwenye kiti cha ubunge katika chaguzi zijazo.

“Na tuongeze idadi ya wanawake kwenye bunge la kaunti kama wawakilishi wa wadi,” alisema Bi Masito.