Makala

Kinaya Ruto akitajwa maarufu ulimwenguni ila nyumbani ni malumbano

January 3rd, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN  

HUKU Wakenya wengi wakimlaumu Rais William Ruto kwa kuondoa hitaji la viza kwa raia wa kigeni wanaozuru Kenya, Jarida la New African Magazine limemtambua kwa hatua hiyo miongoni mwa sababu nyingine.

Rais Ruto ametajwa kuwa mmoja wa Waafrika wenye ushawishi mkubwa mwaka wa 2023 katika makala ya kwanza ya jarida hilo.

Haya yanajiri mwezi mmoja baada ya jarida lililo na makao yake Amerika, ‘Time Magazine,’ kumuorodhesha miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.

Mnamo Desemba 12, 2023, katika maadhimisho ya Jamhuri Dei jijini Nairobi, Rais alitangaza kuwa raia wa kigeni wanaoingia nchini hawatahitajika kuwa na viza kuanzia Januari 2024.

Rais Ruto alisema hatua hiyo inalenga kuboresha sekta ya utalii nchini.

Kadhalika, Jarida la New African limemtaja Rais Ruto kuwa kiongozi anayeheshimiwa na mwenye mvuto licha ya changamoto.

“Nchini mwake (Kenya), uongozi wake umekabiliwa na pingamizi na umaarufu wake umeanza kudidimia lakini amekumbana na maandamano yaliyosukumwa na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga,” lilisema jarida hilo ambalo kadhalika limesifu mipango ya Dkt Ruto ya kupunguza mzigo wa malimbikizo ya madeni ya kimataifa.

Dkt Ruto ametambuliwa siku chache baada ya Waziri wa Fedha Prof Njuguna Ndung’u kutangaza kuwa serikali imelipa $68.7 milioni, sawa na Sh10 bilioni, za riba ya mkopo wa Eurobond.

“Tangu Julai 2023, serikali inaendelea kutekeleza mpango madhubuti wa ulipaji wa madeni ambao unahusisha kiasi cha mapato na mpango wa makubaliano nafuu ya ulipaji huo,” alisema Prof Ndung’u mnamo Desemba 28, 2023.

Hii ni baada ya Ethiopia kukosa kulipa sehemu ya deni ambayo ni kuponi ya dola 33 milioni.

Rundo la madeni nchini limepita Sh10.189 trilioni kuashiria kuwa mwaka mmoja wa serikali ya Kenya Kwanza umeshuhudia kupanda kwa ukopaji.

Mnamo Juni, 2022 deni la taifa lilikuwa Sh8.579 kwa mujibu wa takwimu za Hazina ya Kitaifa.

Kuongezeka kwa madeni kutazidisha mzigo mkubwa kwa mlipashuru sababu ya kuongezeka kwa masharti ya kulipa madeni ya kimataifa haswa riba huku thamani ya Shilingi ikiendelea kushuka.

Tangu Rais William Ruto kushika hatamu za uongozi Septemba 2022, serikali yake imeongeza misururu ya ushuru iliyoishia kuongeza bei za bidhaa muhimu kama vile unga wa ugali, mafuta ya kupikia, sukari, umeme, bidhaa za petroli na kadhalika.

Kujibu shutuma kutoka kwa Wakenya kuhusu sera zake, Rais amerejelea mara kadhaa kuwa maamuzi yake hayatafurahisha wengi lakini yanalenga kujenga mustakabali wa nchi.