Habari Mseto

Kinaya Sportpesa kutuzwa na serikali kisha kuzimwa

July 14th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

NIA halisi ya serikali kupiga marufuku kampuni za uchezaji kamari nchini, imeanza kutiliwa shaka kutokana na maelezo ya sababu zake kukosa umakinifu.

Hii ni baada ya wananchi kushangaa kwa nini kampuni ya SportPesa ni miongoni mwa zinazodaiwa kukiuka sheria za ulipaji ushuru ilhali ilituzwa na Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA) kama mlipaushuru bora zaidi mwaka uliopita.

Hatua ya kuzima kampuni hizo imesababisha kusimamishwa kazi kwa wafanyikazi wa kampuni husika, suala ambalo limetilia shaka kujitolea kwa utawala wa Jubilee kuwasaidia vijana kupata kazi.

Kampuni hizo za kamari hasa Sportpesa na Betin pia zimekuwa mstari wa mbele kufadhili michezo nchini, jambo ambalo litapata pigo kubwa ikiwa serikali haitabadilisha uamuzi wake.

Hatua hiyo itaathiri zaidi vijana ambao ndio hushiriki michezo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa SportPesa, Bw Ronald Karauri jana alisisitiza kampuni hiyo haijakiuka sheria zozote za ulipaji ushuru na inatumai kurejelea biashara yake hivi karibuni.

“Tumejitolea kushauriana na wadau wote husika ili tupate suluhisho litakalofaa pande zote mbili na kusaidia serikali kwenye ajenda zake za maendeleo na pia kutoa nafasi kwa mandhari bora ya kufanyia biashara,” akasema Bw Karauri kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Kando na madai ya kutolipa ushuru, serikali pia imekuwa ikidai inachukua hatua kali dhidi ya kampuni za kamari ili kulinda masilahi ya maelfu ya vijana waliotekwa na michezo hiyo kwa kiwango cha kujiharibia maisha.

Lakini wananchi kwenye mitandao ya kijamii walitilia shaka sababu hizi na kutaka serikali ijitokeze wazi kueleza sababu halisi ya kupiga marufuku kampuni hizo 27.

Mapema mwaka huu, KRA iliibua madai kwamba kampuni hizo zilifaa kulipa ushuru wa mabilioni ya fedha zinazoshindwa na wachezaji.

Mnamo Jumamosi, Rais Uhuru Kenyatta alisema serikali haitalegeza msimamo wake kwa kuwa hatua zilizochukuliwa ni kwa manufaa ya nchi.