Makala

KINAYA: Usimlaumu 'Muthamaki' kwa kufungua kizahanati cha kijijini

December 8th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

USIMLAUMU ‘Muthamaki’ kwa kufungua kizahanati cha kijijini.

Mimi ninamwelewa vizuri sana.

Wakazi watapata tiba – hata ikiwa ni Panadol tu – naye atakoroma na kusikika.

Tangu hapo tunajua ng’ombe akivunjikia mguu malishoni hurejea zizini kusaidiwa.

Masuala ya kitaifa yamemkalia vibaya, hapati fursa ya kupumzika.

Na kwa sababu nyumbani ni nyumbani kungawa pangoni, fursa kama hii, japo inaonekana duni, ikitokea haina budi kutwaliwa mara moja. Wewe teta tu, hajali.

Tazama hapa: ule mkutano wa Gema ndani ya Ikulu ya Sagana uliosifiwa sana kati ya ‘Muthamaki’ na kinamwana wa mlimani ulimuoteshea magugu badala ya kumzalia matunda.

Ingawa wanasiasa waliohudhuria mkutano huo walipiga picha wakivaa tabasamu bandia kutuonyesha umoja wao, mambo yalibadilika hata kabla ya siku kuisha.

Umoja aliopania kuleta ‘Muthamaki’ haukupatikana, alionuia kunyamazisha eti wafunike kombe mwanaharamu apite hawakufyata, sasa si siri tena kwamba hawamsikizi!

Linalomkera hadi ya kumkera ni kwamba kule mashinani, maeneo ya mlimani anakotaka tuamini ni kwake, kunavuma upepo mkali ukipeperusha bendera ya Dkt Samoei.

Sasa ‘Muthamaki’ hajui amfanyie nini msaidizi wake huyo kwa maana Katiba ya nchi imewaunganisha wote wawili kwenye nyonga kama pacha.

Kinyume na hali livyokuwa kabla ya Katiba hii ya 2010, mkubwa hawezi kumfuta mdogo hata wakihasimiana namna gani kwa kuwa walichaguliwa pamoja. Ndoa ya lazima hii.

Kitu rahisi kabisa anachoweza kufanya ni kumwachia mdogo wake huyo kigoda cha Ikulu, arejee kwao kijijini Ichaweri na kuamua Wakenya wajipange au wapangwe na ‘Husler’.

Lakini kufanya hivyo ni kuonyesha uoga, ambao mwana wa Jomo hangetaka kunasibishwa nao ili asiaibishe babake marehemu, mbeba bakora aliyewatwanga watu!

Hivyo basi? Bora avumilie mpaka miaka miwili na nusu ijayo iishe, aamue atarejea kijijini kukama ng’ombe wake au atanata alipo na kuwa Waziri Mkuu. Angali kijana eti.

Nimekwambia ng’ombe akivunjikia mguu malishoni hurejea nyumbani kusaidiwa kwa kuwa ‘Muthamaki’ hakuwa na lazima ya kwenda kufungua zahanati uchwara.

Alitafuta tu kisingizio cha kujitokeza huko nje, awahutubie watu, aseme kinachomkera, lakini alishindwa kuficha ukweli kwamba mwenyewe aliaibika kufungua zahanati.

Tunapozungumza, anayoweza kudai ni ngome yake kikweli ni eneo la Kiambu, hususan Gatundu Kaskazini na Kusini, lakini kwingineko mlimani hana hakika.

Wakazi wa Kiambu, japo si wote, wanaweza kufa naye, ila wenzao wa Murang’a, Nyeri, Kirinyaga, Nyandarua na hata Meru wanaweza kumpiga chenga.

Kisa na maana? Wanadai hajatimiza ahadi alizotoa wakati wa uchaguzi; ana hasira za mkizi ilhali wanajua ni vitisho tu, hawezi kuwafanyia chochote kati ya sasa na 2022.

Mkutano ulionuiwa kuamua eneo la mlimani litaishughlikia vipi ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) uliahirishwa kiajabu, ila duru zinasema alijua pangechimbika!

Nimekuandikia hapa mara kadha kwamba kina mwana wa mlimani ni watu wa ajabu sana; wao huagana na ‘muthamaki’ anayestaafu wakimpa kura za kipindi cha mwisho.

Wanajiamini hivi kwamba hawawezi kumwachia yeyote, hata ‘muthamaki’ mwenyewe, maamuzi kuhusu hatima yao ya baadaye.

Shika hili na usisahau: anachoweza kufanya Dkt Samoei ili kukosana na kinamwana wa kawaida wa mlimani ni kumtukana hadharani ‘muthamaki’ wao. Vinginevyo, sahau!

 

[email protected]