MakalaSiasa

KINAYA: Utapewa Huduma Namba upende usipende, usishindane na Serikali!

April 4th, 2019 2 min read

NA DOUGLAS MUTUA

IKIWA unaikataa Huduma Namba, jiite mshamba wa kweli. Kuna vita ambavyo huwezi kushinda hata ukizua ubishi kiasi gani.

Tangu hapo zamani ulilazimika kumpisha mwenye nguvu lau sivyo uvunjwe mbavu bure bilashi! Mara hii una uwezo gani wa kumpinga?

Kumbuka nchini Kenya kina yakhe kwa wakubwa ni kama sisimizi, ukimkanyaga afe humwambii pole. Utafikichwa kama sisimizi msumbufu, wala hutaombolezwa.

Na, kama anavyopenda kutukumbusha yule kidomodomo wa Garissa Mjini, hii serikali si ya ‘mama wa mtu’. Itapata inachokitaka, upende usipende.

Angekuwa hai bibi mzaa mama angekwambia ‘hii serikali si bibi yako uichezee kama bembea, utasombwa ukafie mbali!’

Ala! Mbona leo nimekujia juu kiasi hiki, kukuonyesha hutoshi mboga mbele ya watawala uliowaweka madarakani?

Samahani, acha nikupoteze kidogo: Ikiwa wewe ni wa ODM tayari umenitukana na kusema hukuiweka madarakani, eti ni siafu wa mlimani na marafiki zao wa bondeni.

Kwani una tofauti gani nao? Wewe ulikataa kupiga kura na kwa njia fulani ukawa umewawezesha kujiweka madarakani, huwezi kuniambia kitu.

Utaniambiaje ilhali yule mganga wako wa risasi moja amejiingiza ndani ya Jubilee kama mchuzi wa wali, tena anatishia kuubomoa msonge mzima wa Jubilee?

Kwa ufupi, si kwamba nakukatisha tamaa. Hata! Nakupambanulia wazi tu hali halisia ya maisha ya Mkenya wa kawaida.

Nimechochewa na ubaradhuli fulani ambao nimeuona mitandano na vijiweni ninakopitia kupiga sofa na washefa nikitoka kuzumbua riziki.

Lofa fulani ametishia kwamba kwa sababu serikali imekataa kumsaidia kwa chochote, hataki nambari yao! Na akinyimwa huduma zote muhimu? Naye atawanyima kura eti.

Sasa shida kuu iko hapo! Kususia uchaguzi, eti kwa nia ya kuwanyima walio madarakani kura, kutasaidia Kenya na nini? Au, bora zaidi, kutakusaidia na nini?

Tumia akili rafiki yangu: Ukikataa kujiandikisha kuoiga kura kwa sababu eti unang’ang’ana na serikali, ikikunyima huduma nawe uinyime kura, unajichongea.

Walio madarakani sasa hivi, ambao kwa hakika hawafanyi kazi ya kuridhisha, wana uwezo wa kuwalipa vibaraka wao wajitokeze pekee kuwapigia kura ukisusia uchaguzi.

Hivyo basi? Wanaweza hata kuwashawishi vibaraka wao kwa mafedha, wapige kura ya kuibadili katiba ili kuirejesha nchi katika siasa duni za chama kimoja – baba na mama.

Hii Kenya, amini usiamini, inahitaji mchango wa kila kitu ili, hata ikiwa si kukua, kuhakikisha hatutumbukii kaburini tunamochungulia wakati huu.

Vinginevyo, tutazikwa na matajiri ndugu yangu, tusahaulike kabisa huku wakiendelea kudumu madarakani.

Acha uzembe, nenda kachukue hiyo Huduma Namba uitie mfukoni na kusubiri siku njema itakayokucha tuwatimue nguruwe wenye kichaa wanaotunyanyasa na kutucheka.

Huwezi kwenda vitani mikono mitupu huku ukitarajia kushinda; huko ni sawa na kujitia kitanzi. Uhai wako ni muhimu, Kenya inakutarajia.

Najua kuna watu wanaoeneza propaganda eti hiyo Huduma Namba ndiyo mwanzo wa ile nambari ya mpinga Kristo, yaani 666, iliyotajwa kwenye Biblia takatifu.

Nenda kamwambie aliyekusomea Biblia juu-chini unajua kujisomea ikiwa wima na kuielewa. Mbona hakukwambia nambari yako ya kitambulisho ni 666? Usikubali kuchezewa akili na mtu, una zako.

[email protected]