Makala

KINAYA: Wabunge wajilipe vinono, nasi pia watulipe kabla ya kutwaa kura zetu

July 13th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

DUNIANI kuna watu wacheshi!

Juzi nusra mtani wangu wa kisiasa anitegue mbavu kwa falsafa ya kuaibisha na kushangaza ila aliyoaminia fika ya kuiaminia.

Mkazi huyo wa eneo kavu la Ithanga, Kaunti ya Murang’a, aliniambia juhudi za kuwashinikiza wanasiasa watufanyie maendeleo zimeshindikana.

Hazina tija eti, watu watafute jingine la kufanya ili kutatua matatizo yao badala ya kuwasubiri waongo waitwao wanasiasa.

Alishikilia kuwa tusipojiamulia hatima ya maisha yetu tutakufa maskini.

Ninaposema ‘sisi’ ninawarejelea kina nani? Wewe nami, watu ambao hawalipwi kuwakilisha watu.

Nilisubiri kwa hamu na ghamu unavyosubiri wewe sasa hivi kusikia mtani wangu huyo alikuwa na mpango gani wa kupata maendeleo.

Aliniambia nisitie shaka, nikalie jamvi anidokezee kuhusu mkakati mpya ambao aliamini utafanya kazi kikweli, tena wenye matokeo ya papo hapo. Hamna kusubiri.

Mtamba hadithi huyo alianza kwa kuniambia eti kadi yangu ya kura ni muhimu sana, ina nguvu zisizo za kawaida.

Khaa! Mambo gani haya! Unadhani nimesikia maneno kama haya mara ngapi? Unataka kuniambia ni mara ya kwanza kudanganywa eti kura yako inaweza kuajiri au kufuta mtu?

Hata! Kila wakati uchaguzi ukifanywa wewe maskini huzidishi hupunguzi, unabaki kaduwaa ukijiuliza nguvu zimekwendapi!

Sote tumetesekea mno katika nchi hii ya ‘kitu kidogo’ ambamo maskini hana haki, mto wa mamba na papa ambapo maji hunywewa na wanyama wenye pembe pekee.

Mwenzangu aliniambia kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2022 zikifika, kila mwananchi anapaswa kukataa kutumiwa kama kiko cha kupakulia kisichofaidi mchuzi wenyewe.

Kazi rahisi eti, yaani kusimama kidete na kumtamkia mwanasiasa kaulimbiu: ‘Leta pesa kwanza, maendeleo kila mtu akafanye kwake!’

Alisema mbinu hiyo itahakikisha kwamba tumemalizana mapema na matapeli waitwao wanasiasa, ambao wamezoea kukimbia na madeni yetu ya maendeleo.

Nilishtuka na kumuuliza iwapo hakuogopa matoeko ya mbinu hiyo kisheria, mathalani adhabu kali kwa anayetoa na anayepokea hongo hiyo.

Aliangua kicheko cha kishetani akaniuliza ninaishi dunia gani kiasi cha kutojua sheria za Kenya zinaishia kwenye vitabu tu, hazitekelezwi.

Alinipa changamoto eti nimthibitishie kwamba wanasiasa waliochaguliwa mnamo 2017 hawakumwaga pesa ili kuzoa kura, akasema tuhalalishe muamala huo ili watu wajipange.

Hoja zake hizo, japo za ajabu kwelikweli, zilinipa kujikuna kichwa, nikajiuliza maswali kadhaa ila kuu lilikuwa iwapo wabunge wanapaswa kuongezewa marupurupu.

Nilijijibu kimyakimya, nikajiambia tuwape marupurupu wanayotaka, tuwawezeshe kuja kununua kura, nasi tuziuze ghali zaidi, mnunuzi na muuzaji waagane roho safi.

Kisha? Kila mtu achanganye nyayo kwenda kwake kuangalia ataanzia wapi kujifanyia maendeleo. Halafu? Ukifuja zako ujilaumu mwenyewe.

Niliafikia uamuzi baada ya kutafakari na kugundua sisi watu wa chini ni bure kabisa! Hatufai! Tunastahili adhabu kali ya kazi ngumu na viboko makalioni!

Tunawajua watu wazuri wanaoweza kufanya kazi za ubunge kwa robo ya mishahara tunayowalipa wabunge wa sasa, tena kazi safi kwa moyo wa dhati, lakini hatuwachagui.

Kwa kuwanyima kura hao tunaodhani ni maskini, wasio na mifedha ya kuwahonga hata majaji na mahakimu, basi tuhalalishe haramu hii ili mkata naye apate.

 

[email protected]