Kinaya wabunge wakitafuna minofu huku wakidai CDF

Kinaya wabunge wakitafuna minofu huku wakidai CDF

NA WAANDISHI WETU

MAMILIONI ya pesa za umma jana yaliendelea kupotezwa kwa siku ya pili ambapo zaidi ya wabunge 300 waliamua kususia mkutano wa siku tano ulioandaliwa katika hoteli ya kifahari Mombasa.

Huku wakidai kutetea maslahi ya wananchi kwa kutaka serikali ya kitaifa iwasilishe fedha za Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF), wabunge hao walionekana wakizururazurura tu huku wengine wakijipumbaza katika mandhari shwari ya Pwani.

Baadhi yao walikiri kwamba serikali imetumia mamilioni ya pesa za umma kuandaa kikao hicho cha mafunzo ya wabunge wa kitaifa.

Ilivyo desturi, fedha za umma hutumiwa kugharimia safari zao hadi Mombasa, makazi, vyakula, malipo ya ukumbi wa mikutano, marupurupu, miongoni mwa mahitaji mengine.

“Watoto wengi hawajaenda shuleni kwa kukosa karo ilhali tuko hapa kwenye hoteli ya kifahari. Hatuwezi kukubali watoto wetu wateseke kama sisi tunajiburudisha hapa,” akasema mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu NG-CDF, Bw Musa Sirma.

Kulingana nao, serikali ilituma Sh7 milioni pekee ilhali walikuwa wakitarajia kupokea Sh50 milioni ambazo zingetumiwa kwa basari za muhula huu.

Bw Sirma alisema uamuzi wao wa kususia mikutano hiyo ni kwa minajili ya kuonyesha kutoridhishwa kwao.
Wakiwa wameungana bila kujali pande za kisiasa, walimlaumu Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung’u, wakidai ndiye anayefaa kutatua suala hilo.

“Amekuwa akiahidi kwamba tutapokea pesa lakini kufikia sasa hakuna pesa zimetumwa kwa akaunti za maeneobunge. Sisi tuko hapa tukitumia mamilioni ya pesa katika hoteli hii ilhali wanafunzi na wazazi wao waliotupigia kura wako nyumbani wakikumbwa na umaskini,” akasema Mbunge wa Marakwet Magharibi, Bw Timothy Kipchumba.

Mbunge wa Yatta, Bw Robert Basil, alisema watasusia pia vikao vya bungeni hadi serikali itoe pesa za NG-CDF.

Aliikosoa serikali kwa kuandaa mkutano huo wa wabunge wakati ambapo kuna mahitaji mengine yanayohitaji kutatuliwa kwa dharura.

“Watoto wa matajiri wako shuleni ilhali wale wa maskini wako nyumbani. Mbona utumie mabilioni ya pesa kuleta wabunge hotelini ilhali watoto wetu wako nyumbani,” akasema.

Mbunge wa Wajir Kaskazini, Bw Ibrahim Saney, alisema hatua ya wabunge hao ilifaa ili malalamishi yao yasikike kwa niaba ya Wakenya.

“Eneo ninakotoka kuna changamoto za ukame, mifugo inaangamia na sasa watoto katika eneobunge langu ni lazima wasaidiwe kurudi shuleni,” akasema Bw Saney.

Suala kuhusu NG-CDF limekumbwa na utatanishi kwa muda mrefu, baadhi ya wanaharakati wakidai hazina hiyo ni haramu Kikatiba. Msimamo huo ulipitishwa pia na Mahakama ya Juu mwaka 2022.

Hata hivyo, wabunge walipuuza agizo hilo na kudai kuwa lilitolewa kwa msingi wa hazina ya zamani ya CDF ambayo, kulingana nao, ilishafanyiwa marekebisho ya kisheria ndipo ikawa NG-CDF.

Katika baadhi ya hotuba zake, Rais William Ruto alitetea msimamo wa wabunge na kuahidi kwamba serikali yake itaendelea kutengea hazina hiyo fedha.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Majangili waendelea kuhangaisha Wakenya...

Ugaidi watishia tena juhudi za kufufua utalii kisiwani Lamu

T L