MakalaSiasa

KINAYA: Wafuasi wa Samoei watatambua Murathe ni nani, watajua hawajui!

December 28th, 2018 2 min read

NA DOUGLAS MUTUA

MAMBO vipi mtu wangu? Krismasi umekula vizuri? Mwaka nao unakuishiaje? Wangu ni vilevile tu, yaani kisiasa, kwa maana kwangu siasa ni uhai.

Siishi kuwacheka walio na ugumu wa kutumia akili na vilevile wanaozitumia visivyo kama kofia.

Juzi nusura niteguliwe mbavu na kicheko kilichozuliwa na wafuasi wa Bill Kipchirchir Samoei, yule ‘kijana wa kutangatanga’.

Wameguswa pabaya, yaani anapoguswa nyati akapandisha mori, wakajipata wakiulizana ‘huyu Murathe ni nani!’

Kisa na maana ni kwamba kiongozi huyo wa Jubilee amesema Bill Samoei na Ouru wametawala pamoja, eti asahau urais kabisa kama alivyosahau titi la mama yake.

Hivyo? Bill aabiri matatu za kwao, aelekee Sugoi naye Ouru aelekee Gatundu ifikapo 2022.

Murathe amesisitiza iwapo kuna makubaliano ya kisiasa kuhusu uungwaji mkono wa Bill Samoei na kina mwana wa mlimani, basi ni kati yake na Ouru, si jamii nzima.

Hilo, kwa hakika, limewauma sana wafuasi wa Bill Samoei. Wanasema Murathe ana kura moja tu. Wasiomjua naibu mwenyekiti huyo wa Jubilee wanauliza na kurudia yeye ni nani!

Nina jibu la swali hilo: David Wakairu Murathe alikuwa mbunge wangu kati ya 1997 – 2002, na ni rafiki wa chanda na pete wa mwenyeji wa sasa wa Ikulu. Anajua mengi.

Mjuaji huyo nusura apoteze wadhifa wake wa ubunge mapema 1998! Ilisemekana kutokana na kuishiwa na fedha kwa kufadhili kampeni yake ya 1997, alitafuta mkakati.

Mkakati wenyewe ulihusisha ‘kumuuzia’ kiti chetu hicho mpinzani wake mkuu, Samuel Kamau Macharia, mmiliki wa sasa wa Royal Media Services.

Duru za kuaminika zilionyesha kwamba Murathe alipewa Sh10 milioni ili ajiengue, kisha amuunge mkono Macharia katika uchaguzi mdogo ambao ungefuatia.

Na alimwandikia Spika wa Bunge, Francis ole Kaparo, kumjulisha kwamba hakutaka kuendelea kuwa mbunge tena.

Lakini barua hiyo ilifuatiwa kwa karibu sana na nyingine ya kuikanusha, yaani kusema eti Murathe hakuiandika yeye hiyo ya kwanza!

Kaparo alifanya uchunguzi wake na kujua kwamba barua zote mbili zilitoka kwa Murathe, akawa na afua mbili: kukitangaza wazi kiti cha Gatanga au kumsamehe mkosaji mjanja.

Lakini wakati uo huo kitu fulani kilifanyika: Mbunge mteule wa Githunguri wa wakati huo, Bw Njehu Gatabaki, alikuwa amekataa katakata kula kiapo cha uaminifu kwa Mzee Moi.

Njehu na Murathe ni mashemeji, hivyo Spika Kaparo angeamua wote waende nyumbani, familia moja ingekabiliwa na bahati mbaya ya chaguzi mbili ndogo kwa wakati mmoja.

Kaparo, kutokana na utu wake kama mzee mwafrika, aliamua kuwasamehe wawili hao baada ya kumshawishi Bw Gatabaki kuapa kama wabunge wengine.

Murathe aliponyoka hivyo, Macharia akapeleka malalamishi mahakamani kisha akashindwa na hatimaye kupeleka kilio nyumbani.

Murathe aliendelea kufoka eti kiti cha Gatanga si cha kupigwa mnada, lakini miaka michache baadaye alikuwa radhi kukitoa kama sadaka ya kisiasa.

Ilipobainika wazi kwamba Mzee Kirungu alitaka Ouru amrithi hapo 2002, Murathe alitangaza kwamba alikuwa tayari kujiuzulu ubunge wa Gatanga!

Kisa na maana? Ili Ouru awanie kiti hicho, akichaguliwa tu ateuliwe makamu wa rais kwa mujibu wa Katiba ya wakati huo.

Ukizingatia haya, utaacha kupuuza anachosema Murathe kuhusu urithi wa Ouru.

[email protected]