Makala

KINAYA: Wajanja hawa wanasiasa, usiwatie maanani la sivyo watakukoroga akili

December 29th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

KENYA haina wanasiasa, ni waigizaji tu.

Ni watu ambao mienendo yao inaweza kutabirika.

Kwa mfano, ninaweza kukutabiria na nikakuapia Jalali kwamba kati ya sasa na wakati wowote ule, mzee-kijana wa Tseikuru hatakuwa na msimamo kuhusu chochote.

Vilevile, ninaweza kukutabiria bila kukosea kwamba ‘Baba’, mradi hajalala Ikulu kama mwenyeji, atakuwa mbioni kuitafuta njia ya kuenda huko kila wakati.

Na bila shaka – tangu ‘Ouru’ apate kipindi cha pili akishindana naye mwenyewe hapo Oktoba 26, 2017 – ninaweza kukutabiria kwamba atakuwa mpatanishi wa nchi.

Kwa nini mpatanishi, tena kuanzia wakati huo? Mgawanyiko wetu haumwongezei sufuria la sima, unamkosesha usingizi tu.

Na umoja wetu? Unawazubaisha wajuaji kama ‘Baba’ na kumpa fursa ya kujifanyia mambo anayotaka bila kuulizwa na yeyote.

Hapo sasa ‘Baba’ ni kama jibwa na mnofu mnono unaolizuia kubweka, naye Wiper ni kama jingine lenye mfupa mkubwa, unazosikia tu ni kelele za meno yakiuvunjavunja!

Hali ikiwa hiyo, yaani ya utulivu na ukosefu wa kelele, ‘Ouru’ anaweza kukopa, bila kubughudhiwa, kwa Wachina watakaotuteka kama rehani tukishindwa kuwalipa.

Wakati huo ‘Ouru’ atakuwa wapi? Usiulize kwa maana sina hakika ninachojua tu ni kwamba wakuu wakistaafu wanapawa heshima zao zote, hawaguswi na mtu.

Kwa hivyo? Madeni ya watu tutalipa bila shaka, tupende tusipende! Na wakuu wa upinzani waliokaa kimya tukikopa tusivyolipa watakuwa wapi? Anayejua ni Mungu.

Hebu angalia wakuu hao walivyomaliza mwaka vizuri, tena kwa njia ya kutabirika. Wiper ametafakari akajua Ikulu halali hata kwa dawa!

Hivyo? Anatafuta mbinu za kutokuwa mbali nayo, hata kama ni kuruhusiwa kuzuru huko kukiwa na karamu, au hata kupita hapo karibu tu aione paa na kusema aliwahi kuota akilala humo.

Ni kwa sababu hii ambapo ameapa kumuunga mkono yeyote atakayeungwa mkono na ‘Ouru’ kumrithi ifikapo 2022.

Hii ina maana kwamba, iwe ni Bill Samoei au Agwambo, ‘Ouru’ atamwambia ampe Wiper japo kifupa kidogo kigumu atafune polepole kabla ya kustaafu siasa na kurejea Tseikuru.

Yaani Wiper amefanya kitu ambacho huwaudhi matajiri wengi mtu anapofika kwao na kuwaambia yuko radhi kufanya kazi yoyote ile, yenye utaalamu au la.

Huyo sasa ni wa kutumiwa, hata ukimpa ndoo yenye mashimo umwambie akujazie tangi kwa maji yaliyo umbali wa maili kumi na mshahara ni Sh2 hawezi kukataa.

‘Baba’ naye amemaliza mwaka kwa mtindo uleule wa kunena makuu akitaka tusadiki ni ya nchi ilhali ni ya kwake mwenyewe.

Tunajua yeye ndiye baba wa Ripoti ya BBI, ndiyo maana amesema mwaka ujao tutaijadili kwa taadhima kuu ili tupitishe kwani ni kitu kizuri. Ikiwa una akili unajua anasema nini.

Je, ulimsikia ‘Ouru’ akimlia mwendazake Charles Rubia? Amesema tuwaige wazee wetu kwa uzalendo, tuviachie vizazi vijavyo nchi bora zaidi.

Kwa njia gani? Eti ushirikiano, umoja na mambo mengine makubwa ambayo hutamkwa na wajanja wakitaka kukugandisha wafanye mambo yao bila kusumbuliwa.

Ukweli ni kwamba miaka ambapo marehemu Rubia na wenzake walitetea siasa za vyama vingi nchini waliitwa wasaliti, wahaini, wasiopenda amani na umoja wa nchi.

Usiwasikilize sana wanasiasa, watakuroga akili.

 

[email protected]