Makala

KINAYA: Wanaokopa bila kutujulisha hawafai kutushurutisha kulipa bila sababu

September 1st, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

NATAKA nikuudhi kidogo. Naam, kwa sababu mwenyewe umeniudhi. Maudhi yako yanaleta heshima ndogo, hufai kuwafanyia watu hivi bwana.

Kwa nini umeniongeza kwenye kikundi chako cha WhatsApp, eti tukuchangie pesa za harusi ya rafiki yako, ilhali sikujui wala simjui? Umeitoa namba yangu wapi?

Mara nyingine ukitaka kufanya hivyo, kwanza hakikisha unayeongeza kwenye hivyo vikundi vyako vya kutiliwa shaka si mimi, lau sivyo nitakuaibisha. Tusizoeane tafadhali.

Ukinipata katika hali nzuri nitakunyamazia tu, niketi hapo kana kwamba sipo mpaka tarehe ya mwisho ya mchango unitoe kwa kutokuchangia.

Watoto wa mjini wanakuita kuhamishwa nyumba inapopakwa rangi maanake sifurukuti hata watu wakinirai namna gani. Zangu huchumia juani, sikupi ukalie kivulini.

Msomaji, nina hakika umewahi kujipata ukiteta hivyo, japo kimoyomoyo, kwa kujipata kwenye vikundi vya michango usiyojua wahusika wala itakavyotumika.

Usijilaumu kwa kuudhika, kila ninayezungumza naye kuhusu suala hili ana malalamiko kama hayo.

Kuna watu ambao wameamua kutuhangaisha bure.

Ajabu, ukithubutu kuwauliza maswali yoyote kuhusu wanavyonuia kutumia pesa hizo au ujaribu kufuatilia iwapo hakika zilitumika zilivyokusudiwa, mnakosana.

Hata utatukanwa! Na usipokoma utapigwa. Kupigwa hasa, kwa sababu ya pesa zako mwenyewe ulizotoa au unazokusudia kutoa.

Hivyo ndivyo jamii yetu ilivyogeuka; matapeli wasiotaka kuwajibikia matendo yao, wanaochukia walio na uthubutu wa kuwawajibisha.

Uadilifu leo hii ni ufala; ucha Mungu ni ‘upumbavu’ pia kwa mizani ya Wakenya wa tabaka mbalimbali.

Na tunapiga domo mchana kutwa tukiwalaumu viongozi wetu eti wamechukua Eurobond na misaada ya kimataifa wakaitumia vibaya badala ya kazi iliyokusudiwa.

Ni wapi kwingine ambako umewahi kusikia watu wakichangisha pesa za mazishi na kuingia mitini huku maiti ikiwa bado kwenye hifadhi?

Ni wapi kwingine ambako umewahi kusikia mtu anadanganya eti jamaa zake – mmoja baada ya mwingine – wamefariki mpaka wanakwisha, akaja kunaswa anaposahau na ‘kumuua’ tena ‘aliyekufa’ awali?

Hiyo ni tabia ya Kikenya, labda Kiafrika pia, na ndiyo sababu unaona sasa viongozi wanazichangamkia fursa za kufanya kazi na Wachina.

Mchina akikupa mkopo hafuatilii kujua umekwenda kuutumia ulivyomwambia au la, hata ukiwapelekea mkeo na watoto mponde raha hajali mradi utamlipa siku ikifika.

Si ajabu viongozi wetu wanaendelea kutajirika huku wananchi wengi wakiendelea kukosa chakula na mavazi.

Tatizo kuu ni kwamba anayedaiwa si mwizi aliyekwenda kuponda raha na mkewe bali mimi na wewe ambao hatuna sauti ya kutosha kuuliza ziliko pesa zenyewe.

Hali si hiyo tunapokopa kutoka mataifa ya magharibi. Hayo makali mno! Yanataka kujua nchi italipa mkopo vipi, ziada mkopo wenyewe utumike ulivyokusudiwa.

Kununua kasri za kifahari kwenye mataifa ya kigeni na pesa zetu kisha siku ya kulipa ikifika maskini wadaiwe ni wizi wa mabavu.

Ajabu akidi ni kwamba Mwafrika aliyenyanyaswa miaka hii yote anamtetea mtesi wake; eti sisi ni taifa huru lisilopaswa kushurutishwa jinsi ya kutumia mali yake na yeyote.

Mkopo wa taifa zima si mali ya mtu binafsi, ni lazima mambo yawekwe wazi ili tusihujumiane, waambie hivyo wanaokopa kwa niaba yako na kukuficha ukweli.

 

[email protected]