Michezo

Kinda ghali zaidi duniani atua Atletico

July 11th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

KINDA Joao Felix ndiye mwanasoka mwenye thamani kubwa zaidi wa umri mdogo duniani baada ya kusajiliwa na Atletico Madrid kwa Sh17 bilioni akitoka Benfica.

Kadhalika, chipukizi huyo ametajwa kuwa mchezaji mahiri zaidi kutoka Ureno baada ya Cristiano Ronaldo anayechezea klabu ya Juventus kwenye ligi kuu ya Serie A nchini Italia.

Felix aliye na umri wa miaka 19 alianza kuichezea Benfica msimu wa 2018-19 katika ligi kuu ya Primeira, lakini akaifungia mabao 15 pamoja na kutoa pasi tisa zilizozaa mabao mbali na kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Kinda huyo alishangaza dunia alipofunga hat-trick dhidi ya klabu ya Eintracht Frankfurt katika pambano la Europa League mwezi Aprili na kuwa mchezaji wa umri mdogo kufungia klabu hiyo mabao matatu katika michuano hiyo.

Mara tu kipaji chake kilipoanza kuonekana hadharani, Felix alianza kuvutia klabu kubwa kama vile Manchester United na Manchester City kabla ya Atletico Madrid kumnunua kwa bei ghali na kumfanya kuwa mwenye thamani kubwa kwa wanasoka chipukizi akimpiku Kylian Mbappe wa PSG ambaye alinunuliwa kwa Sh16.5 bilioni.

Kipaji cha Felix kilianza kuonekana alipokuwa katika shule ya mafunzo ya soka, wakati huo akisakatia timu ya vijana ya FC Porto kabla ya kutimuliwa kwa kuwa alikuwa mwembamba sana ndipo akaamua kujiunga na Benfica.

Mechi ya kwanza

Akiwa na Benfica katika umri huo mdogo mnamo 2016, aliibuka kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi miongoni mwa wachezaji wa ziada kuwahi kuichezea klabu hiyo wakati alipoanza mechi ya kwanza Septemba 2016.

Alianza kuichezea klabu hiyo rasmi msimu wa 2018-2019, mechi ya kwanza ikiwa dhidi ya Boavista mnamo Agosti na katika mechi ya pili alifunga bao lake la kwanza dhidi ya Sporting Lisbon kupitia kwa kichwa, dakika ya 86 baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba.

Klabu wakati huo ilikuwa chini ya kocha Rui Vitoria, lakini alicheza mara kwa mara chini ya Bruno Lage alipofunga mara mbili kabla ya kumaliza msimu akiwa na mabao 20 kutokana na mechi 43 katika mashindano tofauti.

Katika ufungaji wa mabao kwa makinda katika ligi kubwa za Uingereza, Italia, Uhispania, Ujerumani, Ufaransa, Ureno na Uholanzi, Felix akiwa na umri wa miaka 19, alikuwa wa pili nyuma ya Kai Havertz wa Bayern Leverkusen ya Ujerumani.

Vilevile, yuko nyuma ya Mwingereza Jadon Sancho wa Borussia Dortmund kwa upande wa mabao aliyochangia.

Mkufunzi wake wa awali, Carvalhal alithibitisha kwamba alikuwa mchezaji bora zaidi katika shule ya mafunzo ya soka.