Afya na Jamii

Kinda mwenye talanta anayetazamia kuwa rubani wa ndege

May 14th, 2024 2 min read

PETER Njogu ni mwanafunzi wa Gredi ya Nne ambaye moyo wake wa kutoshindwa, uchangamfu na utajiri wa talanta unazidi kuwa kiini cha motisha inayotawala wenzake katika Shule ya Msingi ya St Peter The Apostle Catholic iliyoko Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu.

Safari yake ya maisha ni dhihirisho la ujasiri na dhamira isiyoyumba. Japo alizaliwa mlemavu, hajawahi kuruhusu hali hiyo imzuie kufanya mambo mengi yanayochangamkiwa na watoto wengine kikawaida.

Akiwa mtoto wa pekee wa Bi Carolyne Wanjiru Njogu, Peter alitua katika ulimwengu huu mnamo 2015 tayari akikabiliwa na changamoto za kipekee. Mikono yake, kwa bahati mbaya, haikukua kikamilifu kufikia urefu wa kawaida.

Licha ya mapungufu hayo ya kimaumbile, ari yake ilisalia imara na akakataa kudhibitiwa na mipaka. Akiwa na vidole vitatu pekee – cha shahada, kati na pete – kwenye mikono yake isiyo na vigasha, ulemavu kwa Peter ni kitu ambacho kina nafasi tu katika fikira na mielekeo ya binadamu!

“Ingawa nina mikono mifupi, ninazo ndoto ndefu,” anasema kwa wingi wa tabasamu, akikumbuka jinsi alivyodhihakiwa na kubaguliwa akiwa na umri mdogo.

“Nilipozidi kukua, nilianza kutambua kwamba nilikuwa tofauti na watoto wengine. Upo wakati fulani nilipomuuliza mamangu, ‘Je, ulinyofoa sehemu za mikono yangu? Kwa nini ninaonekana tofauti na watoto wengine?’ Wenzangu wangenikejeli kwa sababu singeweza kucheza kama wao au kushiriki michezo yao.”

Msingi wa kujiamini kwake

Mwanafunzi Peter Njogu akitumia mguu wake wa kushoto kuandikia. PICHA| CHRIS ADUNGO

Peter alianza safari ya elimu mnamo 2020 katika Shule ya Msingi ya Maranatha, Kiambu. Hata hivyo, kuhamia kwake St Peter The Apostle Catholic Nyanjega mnamo 2024 ndiko kulikoweka msingi wa kujiamini kwake. Talanta zake pia zilianza kustawi huku zikikuzwa na walimu na kuchochewa zaidi na wanafunzi wenzake.

“Peter si mwanafunzi tu; yeye ni mwanga wa msukumo kwetu sote. Ukubwa wa ndoto zake zinatukumbusha kuwa hakuna kisichowezekana chini ya jua,” anasema mwalimu wake mkuu, Bw Martin Ekaliani.

Mbali na kuwa wembe darasani, Peter pia ni mtimkaji hodari aliye na kasi ya juu zaidi katika kikosi cha riadha shuleni mwao. Anatamba vilevile katika soka, uchoraji, kuruka mbali, sarakasi na mchezo wa kwata. Isitoshe, amejifundisha kucheza ala mbalimbali za muziki na ni mweledi wa kutumia kompyuta.

Zaidi ya yote, ana shauku, kariha na ilhamu ya kusoma. Hisabati, Kiingereza na Sayansi ndiyo masomo yanayomvutia zaidi. Anapenda pia masomo yanayoegemea kwenye masuala ya sanaa na mawasiliano japo ndoto yake kuu ni kuwa rubani.

“Vipaji hivi vilianza kujikuza ndani ya Peter katika umri mdogo mno. Alipenda sana kuchora. Vyombo vya kidijitali vilimsisimua pakubwa na alivutiwa zaidi na vibonzo na michezo anuwai iliyoshirikisha viwango vya juu vya ubunifu wa kiteknolojia,” anasema Bi Wanjiru.

“Matamanio ya Peter hayana kikomo. Amenifunza kuwa ulemavu si kuzuizi cha ukuu,” anasisitiza mwalimu huyo wa chekechea ambaye pia ni mtaalamu wa elimu tangulizi kwa watoto (ECDE).

Kulingana naye, alipojifungua, familia na baadhi ya jamaa zake walijaribu kumshawishi aache kumnyonyesha mtoto wake wa pekee ili afe kwa njaa. “Lakini nilipenda kile kilichotoka tumboni mwangu, ambacho Mungu aliumba ndani yangu,” anaelezea.

Licha ya mafanikio tele ndani na nje ya darasa, Peter anakabiliwa na changamoto mbalimbali. Kuvalia shati au kufunga zipu ya suruali ni baadhi ya shughuli asizoweza kufanya bila kuhitaji usaidizi akiwa shuleni au nyumbani.

“Kikubwa tunachokifanya ni kuendelea kumhimiza afikie malengo yake. Safari yake inatukumbusha umuhimu wa kukumbatia tofauti za kila mmoja wetu. Sote tumeumbwa kwa mfano wa Mungu,” anasema mwalimu Elizabeth Ndung’u anayemfundisha Peter masuala ya drama.