Habari za Kitaifa

Kindiki aamuru daktari gaidi atumikie kifungo cha miaka 12 kwa kupanga kuangamiza Wakenya

April 27th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amekataa jaribio la kupunguza kifungo cha miaka 12 dhidi ya gaidi aliyepanga kuangamiza Wakenya akitumia sumu ya kemikali ya virusi vya ugonjwa wa kimeta (Anthrax).

Prof Kindiki aliamuru Dkt Mohamed Abdi Ali aliyefungwa na hakimu mkuu Martha Mutuku atumike kifungo chote.

Waziri huyo alikataa kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha Sheria nambari 46 ya Sheria za Magereza kumpunguzia Dkt Ali aliyepatikana na hatia ya kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la ISIS la Iran kifungo hicho.

Waziri alisema Dkt Ali angali hatari kwa usalama wa umma.

Prof Kindiki alisema Dkt Ali hakujutia matendo yake na wala hajaonyesha ishara yoyote ya kubadilika.

“Inafaa Mohamed Abdi Ali asalie ndani na kutumikia kifungo chote hadi akikamilishe,” Prof Kindiki aliagiza katika barua aliyompelekea Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga na Kamishna wa Magereza Brigedia (mstaafu) John Kibaso Warioba,CBS.

Mfungwa huyo alikuwa amepelekwa    kuhudumu katika Hospitali ya Makueni Level 4 mjini Wote 2016.

Alikamatwa na kushtakiwa kuwa mwanachama wa kundi la ISIS na Al-Shabaab.

Alipatikana na hatia ya kuwaingiza vijana katika kundi la ISIS.

Pia alikuwa anatoa mafunzo ya itikadi kali kwa vijana aliowapeleka kupokea mafunzo nchini Somalia na Libya.

Bi Mutuku alimpata na hatia katika mashtaka matano ya ugaidi na kumsukuma jela miaka 12 kwa kila shtaka.

Hata hivyo alimwachilia katika mashtaka matatu.

Kiongozi wa mashtaka Duncan Ondimu alipinga adhabu hiyo akisema “hailingani na uzito wa mashtaka ikitiliwa maanani Ali alikuwa amepanga njama za kutumika virusi vya kimeta kuwaangamiza Wakenya.”

Bw Ondimu alieleza Mutuku kwamba atakata rufaa kupinga uamuzi na adhabu akisema gaidi huyo alistaili kuadhibiwa vikali.

Kufuatia adhabu hiyo DPP Ingonga alimwandikia Prof Kindiki akimsihi asipunguze adhabu hiyo kutokana na ushauri atakaopokea kutoka kwa Idara ya Huduma za Magereza (KPS).

Bw Ingonga alimweleza Prof Kindiki kwamba amekata rufaa na iwapo atampunguzia adhabu mfungwa huyo atatumika siku nane (8) tu kuanzia Aprili 22, 2024, alipohukumiwa.

DPP alimjulisha Prof Kindiki kwamba Bi Mutuku alisema kifungo kianze kutumika Aprili 29, 2016, alipotiwa nguvuni mjini Wote na maafisa wa polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU).

Kabla ya Waziri kutoa mwelekeo DPP aliwasilisha kesi katika mahakama kuzuia KPS kutoa ushauri wa kupunguzwa kwa kifungo hicho.

Jaji Lilian Mutende alizima KPS kutoa uamuzi wa kupunguzwa kwa kifungo hicho cha miaka 12.

Mnamo Aprili 24, 2024, Prof Kindiki alikataa kutumia mamlaka yake kupunguza kifungo hicho na kuwaagiza DPP na Kamishna wa Magereza Brig(mstaafu) John Warioba wawasiliane na Gereza la Kamiti kuamuru Dkt Ali atumikie kifungo chote.

“Gaidi huyu hakughairi matendo yake na hajaonyesha ishara ya kurekebika.Angali hatari kwa usalama wa nchi. Asalie ndani hadi akamilishe kifungo,” Prof Kindiki aliagiza.

Kufuatia agizo hilo, Superitenda Kenrodgers Kyalo Mutemi aliwasilisha afidaviti mbele ya Jaji Lilian Mutende akisema KPS haina wajibu wowote kutetea kesi iliyowasilishwa na DPP akipinga kupunguzwa kwa hukumu kwa vile Waziri wa Usalama wa Ndani amesema Dkt Ali ni “hatari kwa usalama wa nchi na atatumikia kifungo chote.”

Sasa Dkt Ali atasalia gerezani.