Habari Mseto

Kindiki atetea polisi kuhusu mauaji ya mlanguzi sugu wa dawa

April 1st, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

SERIKALI imekanusha madai kwamba ilihusika katika mauaji ya mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya Swaleh Yusuf Ahmed, ambaye pia alikuwa akifahamika kama Kendereni na alikuwa akiendesha shughuli hizo eneo la Pwani baada ya kifo cha Ibrahim Akasha mwaka wa 2000.

Badala yake, serikali ikiongozwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki imehoji kuwa huenda mlanguzi huyo aliuawa na washindani wake.

Vyombo vya usalama vinashuku kuwa Swaleh ndiye alikuwa mlanguzi mkuu wa mwisho, aliyehakikisha kuwa eneo la Pwani lilikuwa na usambazaji wa dawa za kulevya kila uchao.

Mlanguzi huyo aliyeuawa alichukuliwa katika nyumba yake eneo la Kikambala mnamo Machi 8, 2024 saa mbili jioni, na watu ambao baadaye wangemuua na kuutupa mwili wake uliogunduliwa katika kichaka kilomita kadhaa kutoka nyumbani kwake eneo la Kuruwitu, Kaunti ya Kilifi mnamo Machi 16.

Wakati wa kifo chake, Swaleh alikuwa akikabiliwa na madai kadhaa yanayohusika na operesheni za ulanguzi wa dawa za kulevya yenye thamani ya mamilioni ya fedha.

Yeye pamoja na mkewe, Asma Abdalla Mohamed, walikuwa wamehusishwa na ulanguzi huo.

Polisi walikuwa wamefyata mdomo kuhusu suala hilo.

Licha ya hayo, Bw Kindiki amelaumu biashara hiyo isiyo halali kwa kifo chake.

Alizikwa mnamo Machi 17, 2024 katika makaburi ya Sargoi jijini Mombasa katikati ya vurugu zilizolazimu vyombo vya usalama kutuma maafisa wengi wa polisi kutuliza hali.

“Baadhi ya magenge ya kihalifu, hushindana na hata kuumizana. Kwa hivyo hatuwezi kusema,” akasema waziri huyo wakati wa ziara katika kituo cha kurekebisha walioathirika na dawa za kulevya katika eneo la Miritini.

Aidha, wakuu wa idara ya polisi katika eneo la Pwani walihakikishia Taifa Dijitali, kuwa mshukiwa huyo aliuawa na mahasidi wake.

“Bado tunachunguza ila polisi hawakuhusika. Ulimwengu wa ulanguzi huwa hatari sana kwa sababu ya uhalifu unaoendelea humo. Huwa wanaangamizana wenyewe kwa wenyewe kila biashara inapokwenda kombo. Tunafanya uchunguzi zaidi kubaini ni nani aliyemuua,” akasema mmoja wa polisi wakuu katika eneo la Pwani ambaye aliomba kutotajwa.

Prof Kindiki alitetea taasisi za ulinzi akisema kuwa wao hutekeleza shughuli zao kwa kufuata sheria akipinga kuwa suala hilo ni mauaji ya kiholela akihoji kuwa hilo kwa sasa ni kinyume na sheria.

Aliongeza kuwa polisi walikuwa wamepewa mwongozo kutumia nguvu zote kisheria kuwakamata na kutuliza athari zote za usalama wa taifa, ikiwemo ugaidi na ulanguzi.