Kindiki sasa aamua kujiondoa katika siasa baada ya uchaguzi ujao

Kindiki sasa aamua kujiondoa katika siasa baada ya uchaguzi ujao

ALEX NJERU na JURGEN NAMBEKA

SENETA wa Tharaka Nithi Professa Kithure Kindiki aliyependelewa na wengi kuwa mgombea mwenza wa naibu wa rais William Ruto, ameeleza kuwa atajiondoa katika siasa kuanzia Agosti 10.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Nairobi, alieleza kuwa hatahisi kudanganywa kwa kukosa kupewa nafasi hiyo ya kuwa naibu wa rais, iwapo muungano wa Kenya Kwanza utashinda Uchaguzi Mkuu ujao.

Kulingana naye, alimtakia kila la heri mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua aliyeteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto, na hatatafuta hata nafasi yoyote ya kuteuliwa kwa muda.

Bw Kindiki alikosa kuteuliwa licha ya kupendelewa na wengi kuwa naibu wa Dkt Ruto.

“Kura za maoni zilizofanywa zilionyesha nilipendelewa kuliko ndugu yangu. Hatua ya kuacha siasa kwa muda haihusiani na mchakato wa kumtafuta naibu wa rais uliokamilika,” alisema Prof Kindiki.

Licha ya hayo, alieleza kuwa ataendelea kuunga mkono muungano wa Kenya Kwanza, hadi uchaguzi utakapokamilika.

“Nimetosheka na uamuzi wa muungano wetu na nitanyenyekea chini ya uongozi wa Dkt Ruto na Bw Gachagua. Nitamuunga Dkt Ruto mkono ili awakomboe Wakenya kwa kushinda Uchaguzi wa Agosti 9,” alieleza.

Haya yanajiri siku chache baada ya babake seneta huyo ambaye amekuwa katika siasa kwa miaka 22, akifichua kuwa hakumtaka mwanawe awanie kiti cha ugavana.

Kulingana na Bw Daniel Kindiki, hakutaka mwanawe ahusike na uongozi wa serikali za kaunti, kwa madai ya kuhusishwa na ufisadi.

Alieleza Taifa Leo kuwa, hakuwahi kumwelezea mwanawe kutoridhika na hatua yake ya kutafuta nafasi ya ugavana.

“Niliogopa kuwa cheo hiki kingeshusha hadhi ya mwanangu. Sikumweleza aache azma yake. Ni naibu wa rais alimshawishi aungane naye katika siasa za kitaifa,” alisema Bw Kindiki.

Babake Seneta huyo alifichua kuwa kabla ya kujiunga na chuo kikuu cha Moi kusomea uanasheria, alitaka kusomea thiolojia.

“Huyu mwanangu ni mhubiri mzuri. Sijui kama bado yeye huhubiri tangu ajiunge na siasa. Ila ni mkristo wa kujitolea,” alisema Bw Kindiki.

Babake alieleza kuwa seneta huyo ana nidhamu ya hali ya juu na mwenye kuheshimu sheria.Bw Kindiki sasa ameeleza kuwa hatakuwepo kwa nafasi yoyote ya uteuzi, licha ya kupoteza nafasi yake ya kuwania ugavana. Aliacha azma hiyo baada ya Dkt Ruto kumuomba aache azma hiyo na kumuunga mkono.

“Nawaomba watu wa Tharaka-Nithi munipe Kindiki niende tukafanye kazi naye. Twende tukatengeneze serikali ya kitaifa,” alisema Dkt Ruto katika mkutano wa siasa mnamo Februari.

You can share this post!

Safari ya mwaniaji mwenza wa Ruto tangu kijijini Hiriga

Wataalamu waunga Muthama ugavana

T L