Dondoo

King'asti aelezea alivyomhepa mumewe baa na kumlisha polo asali gesti

April 30th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

KAYOLE, NAIROBI

MWANADADA mmoja mtaani hapa alishangaza marafiki zake alipowafichulia kwamba alimuacha mumewe katika baa na kwenda kurushana roho na meneja wa baa hiyo kwenye lojingi.

Yasemekana mwanadada huyo alikuwa akijivinjari na mumewe alipotekwa na hisia za kimapenzi na jamaa ambaye alikuwa akimmezea mate kwa muda.

Aliwaeleza marafiki kwamba haikuwa mara yake ya kwanza kwenda katika baa hiyo akiandamana na mumewe na kila mara jamaa alikuwa akimrushia mistari ya mapenzi.

“Mwanadada alisema siku ya tukio, aliandamana na mumewe katika baa hiyo na wakateremsha vileo hadi akalewa. Walipokuwa wakiendelea na starehe zao, marafiki wa mumewe walifika na wakaanza kujadili mambo yao hadi akaboeka.

Ni wakati huo ambapo jamaa aliyekuwa akimmezea mate alimuashiria amfuate na kwa sababu alikuwa amepandwa na stimu, alimfuata hadi lojingi, wakapapasana na kula uroda,” alieleza mdokezi.

Mwanadada huyo alisema baada ya nderemo kwa nusu saa, alioga na kurudi ndani ya baa ambapo alimpata mumewe akiendelea kuzungumza na marafiki wake.

“Alisema mumewe hakugundua japo binafsi alihukumika moyoni. Alihisi kumchukia jamaa huyo hata kama hakumlazimisha kuchovya asali. Alimuacha mumewe na marafiki zake na kwenda nyumbani,” alisema mdokezi.

Kilichomsumbua zaidi ni kwamba, jamaa hakutumia kinga wakati wa shughuli na alihofia huenda alipata maradhi ya zinaa.

“Ilibidi marafiki zake wamshauri aende kupimwa Ukimwi ili kuwa na hakika hakuambukizwa. Walimweleza kuwa ufuska ni hatari na unaweza kumwangamiza. Mwanadada huyo alijuta na kuacha kwenda baa,” alisema mdokezi.

Hata hivyo, baadhi ya wanawake walimdharau kwa kumsaliti mumewe huku wengine wakimlaumu mumewe kwa kuzoea kumpeleka baa.

…WAZO BONZO…