Kingi afunguka roho kuhusu PAA, uhusiano wake na Raila

Kingi afunguka roho kuhusu PAA, uhusiano wake na Raila

Na PETER NGARE

GAVANA Amason Kingi wa Kilifi ametetea hatua yake ya kubuni chama cha Pamoja African Alliance (PAA), akisema wakati umefika kwa Wapwani kuwa na jukwaa la kutetea maslahi yao jinsi yanavyofanya maeneo mengine nchini.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Gavana Kingi alisema hatua yake inaongozwa na msukumo wa kusaidia Wapwani kujikwamua kutoka kwa matatizo ambayo yamewakumba kwa miaka 58 tangu uhuru, bila wao kupata mtatuzi.

Alikanusha madai kwamba anatumia PAA kwa nia ya kujiweka katika nafasi bora ya kushirikishwa kwenye serikali itakayochaguliwa mwaka 2022, akisisitiza kuwa “amekomaa kisiasa kiasi cha kuweka mbele maslahi ya wakazi wa Pwani”.

“Kama haja yangu ni kuteuliwa waziri katika serikali ijayo singehitaji kujihangaisha na PAA. Ningeenda tu kwa wanaotaka viti vya urais na kutangaza uaminifu wangu kwao. Hakuna siku tumesimama kama PAA tukasema tunataka kiti hiki ama kile. Tunaongozwa na masuala mazito kuliko vyeo serikalini. Mahali nimefika kisiasa nimekomaa kiasi cha kuweka kando maslahi yangu ya kibinafsi kwa ajili ya watu wetu wa Pwani. Mungu ameniweka mahala nipo ili nichangie katika kukomboa wakazi wa Pwani kutokana na changamoto zinazowakumba, na nisipotimiza hili nitakuwa nimepoteza mwelekeo,” akaeleza.

Alifafanua kuwa viongozi wa kisiasa na wataalamu kutoka Pwani wanakubaliana kwa kauli moja kwamba, kuna haja ya kuungana kwa ajili ya kukomboa eneo hilo kutoka kwa matatizo ya ardhi na kiuchumi, lakini kikwazo kikuu ni kuwashawishi wengi wao kuweka kando maslahi yao ya kibinafsi kwa ajili ya jamii nzima ya Pwani.

“PAA sio wazo la Gavana Kingi. Haya ni maono ya jamii ya Pwani. Kabla ya kubuni PAA tulifanya vikao na wabunge na magavana Nyali, Taita Taveta na Nairobi na kwa kauli moja tukatangaza haja ya kuwa na sauti moja. Tatizo lililopo ni kuwa wengi wanatizama zaidi mustakabali wao binafsi kisiasa, na wanaona ni heri kuchukua mkondo rahisi wa kukaa katika vyama vikubwa vya kutoka nje ya eneo letu, badala ya kung’ang’ana kubuni jukwaa jipya,” akasema Gavana Kingi.

Ardhi na Uchumi

Alieleza kuwa malengo makuu ya PAA ni kupigania haki ya ardhi na uchumi wa wakazi wa Pwani.

“Hakuna serikali ambayo imetawala Kenya imekuwa na ujasiri wa kutatua tatizo la ardhi Pwani. Badala yake, suala hili limekuwa chambo cha kutumiwa na wanasiasa wakati wa kampeni, na baada ya kupata vyeo wanatoweka.

“Tatizo la ardhi hapa Pwani lina mizizi yake katika enzi za ukoloni. Wakati wazungu waliteka ardhi maeneo ya Kati na Rift Valley, hapa Pwani ni Waarabu walikuwa wakijigawia mashamba bora hususan yaliyo karibu na fuo za bahari.

“Baada ya uhuru, ardhi iliyokuwa imetwaliwa na wazungu bara ilinunuliwa na serikali ikagawiwa wenyeji, na hivyo ndivyo tatizo la ardhi lilitatuliwa huko. Lakini hapa Pwani, ardhi hiyo ingali mikononi mwa walioitwaa kabla ya uhuru. Ndiposa kila uchao unasikia wakazi wamebomolewa makao na kutimuliwa.

“Kama PAA tutapigania serikali itafute hela inunue ardhi hiyo kutoka kwa wamiliki wake wa tangu ukoloni, ili igawe kwa wenyeji,” akafafanua Gavana.

Bw Kingi alisema shughuli ambayo imekuwa ikiendelea ya utoaji wa hati miliki za ardhi maeneo ya Pwani sio suluhisho, akieleza kuwa serikali imekuwa ikitoa hati hizo katika maeneo ambayo hayana ubishani wa umiliki.

“Hati zinatolewa katika maeneo ambayo hayana tatizo. Shida imo katika ardhi iliyo karibu na ufuo wa bahari,” alihoji.

Kuhusu uchumi, Gavana Kingi alisema serikali ambazo zimekuwepo zimekosa kubuni mikakati mahsusi ya kuwainua Wapwani kiuchumi hasa katika kilimo cha korosho, nazi na zingifuri.

Kuhusu uaminifu wake kwa chama cha ODM ambacho alichaguliwa kwa tiketi yake, Bw Kingi alisema chini ya chama hicho cha kinara Raila Odinga, maslahi ya Wapwani hayajaangaziwa kikamilifu.

“Kama wanachama wa ODM hatuna usemi mkubwa kwani inabidi tufuate msimamo wa chama, hata kama hatukubaliani na baadhi ya maamuzi. Ndiposa sasa tunataka kushirikiana na vyama kutoka maeneo mengine ya nchi ikiwemo ODM kama washirika bali sio wanachama. Hii itatupa nguvu ya kusukuma ajenda za Pwani vizuri zaidi.

“Ndiposa tumesema wakati huu tunataka tuketi na wengine, tusikizane nafasi yetu ni gani katika ushirika wetu nao. Haja yetu si vyeo bali ni kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yetu kama Wapwani, na kuwa na uhusiano ambao utatupa sauti inayoweza kusikika kitaifa. Lazima tupiganie uhuru wa kisiasa wa Wapwani na maslahi ya wakazi jinsi jamii za maeneo mengine zinafanya.

“Kwa muda mrefu Pwani imekuwa kama nyumba iliyo wazi kisiasa, ambapo yeyote anaingia hadi chumba cha malazi na kutoka apendavyo. Lakini safari hii tunasema kuna wenyewe na ukitaka kuingia huku lazima upewe kibali na wenyeji,” akafafanua.

Umoja wa WapwaniKuhusu kibarua cha kubuni umoja wa Wapwani ambao umekuwa ukihepa juhudi za wengi, Bw Kingi alikubali kuna changamoto kubwa, lakini akasema hii ni safari ndefu ambayo sharti walio na maono mema kwa Pwani waitembee.

“Nakiri Wapwani tumeshindwa kushikana kama kitu kimoja kwa muda mrefu. Lakini hii ni safari ndefu ambayo tumeamua kuianza kwa ajili ya vizazi vijavyo. Sio safari rahisi, lakini nina imani kubwa kuwa tutafanikiwa,” akaongeza.

Alifafanua kuwa PAA wanashauriana na vyama vingine vyenye asili ya Pwani katika kuhakikisha wanaingia kwenye uchaguzi mkuu 2022 wakiwa na msimamo mmoja.

“Tutakuwa na sauti kubwa kama Wapwani iwapo tutakubali kuchagua viongozi kwa tiketi ya chama chenye mizizi ya Pwani,” akaeleza.

You can share this post!

IEBC kufanya usajili tena Januari 2022

Kenya yaendea Morocco fainali ya kufa-kupona kuingia Kombe...

T L