Kingi alia kuachwa mpweke kutetea wakazi wa Pwani

Kingi alia kuachwa mpweke kutetea wakazi wa Pwani

Na CHARLES LWANGA

GAVANA wa Kilifi, Bw Amason Kingi amelalamikia jinsi viongozi wenzake ukanda wa Pwani walivyomwacha mpweke kutetea uundaji wa chama kitakachounganisha jamii za eneo hili kabla Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Bw Kingi alisema inasikitisha kuona kuwa wito wa muugano wa Wapwani umekuwa suala la mtu mmoja pekee baada ya viongozi wengine kuanza kusita kujiunga na vuguvugu hilo.

“Nilipotoa wito huu wa umoja wa Wapwani, niliweka bayana kuwa maono haya si ya mtu mmoja wala Gavana Kingi pekee, bali ni maono ya Wapwani baada ya kuteseka kwa miaka mingi chini ya uongozi wa vyama visivyo na mzizi wa Pwani. Tuliona kuwa wakati umetimia wa kujikomboa wenyewe kama wakazi wa pwani,” alisema.

Alikuwa akizungumza katika mazishi ya mwanasiasa mkongwe na mzee wa Kaya, Bw Kahindi Jongolo mjini Mariakani.

Wiki chache zilizopita, wabunge wanaoegemea upande wa Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho na wale wa mrengo wa Tangatanga ambao wanahusiana na Naibu Rais William Ruto, walijitenga na wito wa umoja wa Wapwani.

Tayari Bw Joho na naibu mwenzake wa Chama cha ODM aliye pia Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, wamewasilisha ombi la kutaka kumenyana na Kinara wa ODM, Bw Raila Odinga kupeperusha bendera ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Bw Kingi alisema baada ya kuanza safari ya kuunganisha Wapwani, amekuwa akifanya mikutano na wabunge wa eneo hilo zima lakini wengine wao wamekuwa wakisita kuitikia wito huo.

“Nimejaribu kadri ya uwezo wangu kuleta wabunge wa Pwani pamoja kwa lengo la umoja lakini wengine wao wamekuwa wakisitasita. Tafadhali tuelewane hapa kuwa umoja wa wapwani si maono ya Kingi lakini ya watu wote wa eneo hili ambao wanataka kukomboa Pwani,” alisema.

Bw Kingi alisema mwenendo kama huo unaoshuhudiwa na baadhi ya wabunge huenda ukaleta madhara na hata kusambaratisha maazimio yao ya umoja.

Lakini Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire ambaye ni karani wa Kikundi cha Wabunge wa Pwani (CPG), aliambia Taifa Leo kwa simu kuwa, ingawaje wabunge wa pwani wanaunga mkono umoja wa wapwani, bado wangali na maswali mengi kuhusiana na wito huo wa Gavana Kingi ambayo bado hajawajibu.

“Hatutaki kufuata mwito bila kujua ukweli kisha baadaye tuachwe mataani. Gavana anafaa akuwe mkweli kuhusiana na wito wake,” alisema.

You can share this post!

Wawili wafariki, mmoja ajeruhiwa kwenye shambulio la...

Bensouda sasa ahusisha Ruto na kesi mpya