Kingi aonya wakazi dhidi ya kuuza ardhi na kubakia maskwota

Kingi aonya wakazi dhidi ya kuuza ardhi na kubakia maskwota

Na ALEX KALAMA

GAVANA wa Kaunti ya Kilifi Amason Kingi amewaonya wakazi dhidi ya kuuza ardhi zao kiholela na kuchangia mizozo ya ardhi katika kaunti hiyo.

Akizungumza baada ya kutoa vyeti vya umiliki wa ardhi kwa wakazi wa Chumani, Bw Kingi aliwarai wakazi wa eneo hilo kuzitumia ardhi hizo vyema katika kujiendeleza na wala sio kuziuza kiholela.

“Sitaki kuleta vitu kama hivi kwenu halafu baada ya wiki mbili tupate habari kwamba kati ya zile hatimiliki watu wa Chumani walipata zimeuzwa, manake ukiuza ni lazima uondoke na ukiondoka utatupatia shida nyingine kule unakoenda. Kuna kitu wazungu wanaita Professional Squatters kwa hivyo wakati serikali hii inaenda mbio inaweka pesa kwa sababu ya kutoa suluhisho la ardhi tafadhalini nawasihi tusiwe na urahisi kwamba tumepata vyeti ngoja tuuze,” alisema Bw Kingi.

Kulingana na gavana huyo amewataka wakazi hao kuzikodisha ardhi hizo endapo wanakumbwa na matatizo ya kifedha na wala sio kuuza ardhi hizo kwani huenda baadaye zikawaletea matatizo.

“Kuna kitu kinaitwa leasing – kukodisha – ikiwa mtu kabisa umeshindwa, ni shida kabisa ya hela na kilichobaki ni shamba lako peke yake. Usiuze manake huo ni urithi wako na vizazi vyako vinavyokuja. Hilo ndilo wazo ningetaka niwaachie manake sehemu nyingine tumepeleka hatimiliki mara unasikia wamevunjiwa. Sehemu zile ukifika kule zile sura ulizozipatia hatimiliki umalize shida hii wameenda kututafutia shida nyingine. Wakati tunapotatua shida hii pia na,sisi tujali kwamba hatimiliki si kitu cha kuuza,” alisema Bw Kingi.

Kwa upande wake waziri wa ardhi katika serikali ya kaunti ya Kilifi Bi Maureen Mwangovya amezitaka bodi za kudhibiti uuzaji wa ardhi kuwa makini kabla ya kuruhusu ardhi kuuzwa.

“Kupata hii hati miliki ni muhimu na itakusaidia wewe na kizazi kijacho,lakini ukipata ile hatimiliki ukiuza hata kabla hujaishikilia kidogo huwa yaleta shida katika familia. Hii bodi ya kudhibiti uuzaji wa ardhi ya Kilifi Kaskazini na ni jambo la kusikitisha na haya ambayo ni malalamishi ambayo yanatoka kwa wale wanakamati wenyewe. Ukiangalia Tezo mashamba mengi yameuzwa na ni hali ya kusikitisha. Na Tezo ni jirani na, hapa wewe umepewa hatimiliki iweze kukusaidia wewe kama ni upande wa biashara upeane kama dhamana ili uweze kufanya miradi tofauti tofauti lakini usiuze,” alisema Bi Mwangovya.

You can share this post!

Hakimu asimulia jinsi walivyoponea shambulio

Wizi wa taa, alama za trafiki vyanzo vya ajali – KeNHA

T L