Kingi apuuzilia mbali shinikizo kumtaka ajiunge na Ruto

Kingi apuuzilia mbali shinikizo kumtaka ajiunge na Ruto

WACHIRA MWANGI na MAUREEN ONGALA

GAVANA wa Kilifi, Bw Amason Kingi, amepuuzilia mbali wanasiasa wa Pwani ambao wamekuwa wakimshinikiza aungane na mrengo wa Naibu Rais William Ruto, akiwataka wawe waaminifu katika misimamo yao ya kisiasa.

Bw Kingi, ambaye amejitenga na Chama cha ODM alichotumia katika uchaguzi uliopita, alisisitiza kuwa njia pekee ya Wapwani kujikomboa kisiasa ni kama wataunga mkono mpango wake wa kuunda chama cha Pwani kitakachotambulika kitaifa.

“Hapa Pwani, ikiwa hatutasimama kidete itakuwa kama ya juzi. Kupangwa. Mwenye kisima, hapangi foleni. Sisi twapanga foleni kwa visima vya wenyewe. Ni kitu gani hiki kinatushinda hadi hatuwezi kuchimba visima vyetu?” akasema.

Wiki iliyopita, Taifa Leo ilibainisha kuwa, wandani wa Dkt Ruto katika eneo la Pwani walikuwa wameanza kumwandama Bw Kingi wakimtaka aungane nao ili waingie katika Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Wanasiasa hao walianika wazi nia yao katika mazishi ya Sada Mgalla Nyawa, ambaye ni mamake Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya mnamo Jumanne, iliyohudhuriwa pia na Dkt Ruto.

Akizungumza Jumatano wakati wa uzinduzi wa kitengo cha kina mama kujifungua, na chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Mariakani iliyo Kaloleni, alisisitiza kuwa njia pekee ya Pwani kuwa na usemi katika uongozi wa kitaifa ni ikiwa wenyeji wataungana katika chama chao kimoja.

“Ukiona mawimbi yanatanda, ni lazima ujipange la sivyo mvua itanyesha na utapata huna mbegu, na wakati wa kupanda ukipita itabidi uende kwa jirani kuomba chakula. Safari hii ya 2022 inapangwa kimafungu na kila mkoa ikiwemo Bonde la Ufa, Magharibi na hata maeneo ya kati nchini wanaweka nyumba zao sawa. Hata wenzetu kutoka maeneo ya Kaskazini Mashakari wamechukua hatua kubwa sana kujipanga kisiasa,” akasema.

Gavana huyo anayetumikia kipindi chake cha mwisho cha ugavana, Jumanne alionekana pia kukerwa na jinsi suala la umoja wa Wapwani ndani ya UDA liliibuliwa mazishini, ilhali wanasiasa waliokuwepo walikuwa wameanza naye safari ya kubuni muungano wa Pwani awali kisha wakamwacha pweke njiani.

Imesemekana amepanga kuzindua chama kipya hivi karibuni, baada ya viongozi wa vyama vitano vya Pwani alivyokusudia kuvishawishi viungane, kumtenga na kukataa wito kuwa vyama hivyo vya KADU Asili, Shirikisho, Republican Congress, Umoja Summit na Communist vivunjwe ili kuunda kimoja.

Hivi majuzi, Bw Kingi alionyesha nia ya kuungana na One Kenya Alliance (OKA) alipokutana na vinara wa muungano huo Mombasa ambao ni Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (Amani National Congress), na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford-Kenya).

“Kawaida yangu huwa sizungumzi mambo ya kisiasa mazishini lakini nimesukumwa ukutani. Hatufai kusubiri mazishi ili tukumbushane kuhusu hitaji la kujipanga. Mbona mlisubiri mama afariki ndipo mje hapa kunishambulia? Hii ni aibu. Tukaeni chini pamoja na tushauriane, tusirushiane maneno mazishini,” akasema.

Wanasiasa waliomtaka aungane na Dkt Ruto ni wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Feisal Bader (Msambweni), Benjamin Tayari (Kinango), Kimani Ichung’wah (Kikuyu) na Lydia Haika (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Taita Taveta).

“Gavana Kingi na Mvurya, mlitoka Misri. Nawaomba, huu ni wakati msikilize sauti zasema nini mashinani. Watupige, watusimange, sisi hatubanduki. Msiingie kwa chumba kungonja kupangwa. Twataka tuwe kwa serikali pia sisi,” alisema Bi Jumwa.

Wito wa viongozi hao wa Pwani ulitiliwa mkazo na Dkt Ruto, ambaye alimwambia Bw Kingi kwamba pia yeye si mwanachama rasmi wa UDA lakini amejitolea kuungana na viongozi wanaotaka kuleta umoja na maendeleo kitaifa.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ikabili baa la njaa mapema

UhuRuto wazua wasiwasi