Kingi atumai Ruto hatamruka akishinda urais

Kingi atumai Ruto hatamruka akishinda urais

NA KNA

GAVANA wa Kilifi, Bw Amason Kingi, amesisitiza kuwa anaamini Naibu Rais, Dkt William Ruto, atatimiza makubaliano yote waliyoafikiana alipojiunga na Muungano wa Kenya Kwanza.

Akipigia debe wawaniaji viti kupitia chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA) Kilifi, Bw Kingi alisema Dkt Ruto alitia saini makubaliano hayo kwa hivyo atahitajika kuyatimiza akishinda urais.

Gavana huyo anayetumikia kipindi chake cha mwisho mamlakani alieleza kuwa, Dkt Ruto alikubali kwa maandishi kununulia maskwota ardhi ili kukomesha visa vya kufurushwa kwao mara kwa mara.

Masuala mengine ambayo anatarajia yatatekelezwa endapo naibu rais ataunda serikali ijayo ni kuhusu ufufuzi wa viwanda vya Pwani.

Vile vile, ilibainika kuwa Bw Kingi aliahidiwa wadhifa wa spika wa seneti ikiwa Kenya Kwanza itashinda urais.

Wakati uo huo, Bw Kingi amedai kuwa eneo la Pwani litanufaika zaidi ikiwa wakazi wataunga mkono chama kilicho na mizizi yake katika ukanda huo.

Alieleza masikitiko yake kwamba wakazi wa Pwani wanazidi kufuata vyama vingine ambavyo vinatetea zaidi maslahi ya maeneo mengine ya nchi kuliko ukanda huo.

Kupitia ushirikiano wa PAA na UDA, muungano wa Kenya Kwanza unatazamia kupunguza ushawishi wa kisiasa wa kinara wa ODM, Bw Raila Odinga katika kaunti hiyo.

Bw Kingi na viongozi walioandamana naye kwenye mikutano ya hadhara walimkashifu Bw Odinga anayewania urais kupitia Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, wakidai kuwa hana shukrani kwa wanasiasa waliomwezesha kupata kura nyingi eneo hilo katika uchaguzi uliopita.

“Hakuna mtu mwingine aliyepigania na kufanyia ODM na Raila kampeni kuliko mimi, lakini sasa nasema imetosha. Hatujakuja hapa kupigia debe ODM wala Baba (Bw Odinga), bali tumekuja kuwazika katika kaburi la sahau,” akasema.

Katika uchaguzi wa 2017, ODM ilizoa kiti cha ugavana, useneta, mwakilishi wa wanawake bungeni, viti vyote vya bunge la kitaifa na idadi kubwa ya madiwani Kilifi.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Utepetevu wa IEBC wakeketa maini...

Raila ashawishi Ngilu kujiondoa kura ya ugavana

T L