Kingi aungama mambo si shwari kwa ODM Pwani

Kingi aungama mambo si shwari kwa ODM Pwani

Na MOHAMED AHMED

KAUNTI ya Kilifi ambayo kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 ilichagua viongozi wote kwa chama cha ODM, imeanza kuyumba na kuchukua mwelekeo tofauti dhidi ya kinara wa chama hicho Raila Odinga.

Kilifi ndiyo kaunti pekee nchini ambayo Gavana, wabunge, Seneta, Mbunge Mwakilishi wa Kike na wawakilishi wadi (MCAs) walichaguliwa kupitia ODM.

Lakini sasa Gavana Amason Kingi ambaye ndiye mwenyekiti wa chama hicho katika Kaunti ya Kilifi, ameingia kwenye kampeni dhidi ya chama hicho, hatua ambayo itakuwa ni pigo kuu kwa Bw Odinga.

Akizungumza katika mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, Bw Kingi alisema kuwa kwa muda sasa Pwani imekosa uwakilishi mzuri katika meza ya kitaifa, kwa sababu ya kuwakilishwa kupitia vyama vingine kikiwemo ODM.

Bw Kingi alisema hayo huku akiweka wazi kuwa hatawania tiketi yaUrais kupitia chama cha ODM.

“Mimi sitawasilisha ombi langu la kuwania kiti hicho kupitia ODM. Hilo liwe wazi kabisa. Azma ya kuwania kiti hicho bado ipo, lakini haitatimia kupitia ODM. Kwa sasa mwelekeo wangu ni kuhakikisha kuwa tunapata chama chetu cha Pwani,” akasema Bw Kingi.

Alisema kuwa mpango wake ni kuhakikisha kuwa vyama vyote ambavyo vipo Pwani vinakuja pamoja na kuwa kitu kimoja, na kusisitiza kuwa ni katika muungano huo ndipo Pwani itaweza kusikika na sio kuendelea kutegemea watu wengine kama vile imetegemea ODM kuwakilisha matakwa yake kwa muda.

Taifa Leo imegundua kuwa kuna mpango wa magavana wa Pwani pamoja na viongozi wengine kutoka kanda hiyo kukutana wiki hii ili kujadiliana kuhusiana na umoja huo wa Pwani ambao umeonekana kubabaisha viongozi.

“Ni kweli kutakuwa na mkutano wa viongozi lakini mpango wetu ni kufanya mambo bila kupiga fujo maana kuna wale maadui zetu ambao wanatishiwa na kuungana kwa Pwani. Hivyo basi, tusubiri tu ndani ya siku hizi chache na watu wetu wataona mwelekeo,” akasema Bw Kingi kuhusiana na mkutano huo ambao unatazamiwa kuleta mwelekeo mpya.

Mwito wa umoja huo umepelekea Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Kilifi Kaskazini Owen Baya kujiondoa katika kumuunga mkono Bw Odinga.

Mbunge wa Kaloleni Paul Katana ambaye pia alipata kiti chake kupitia ODM anavutia upande wa wabunge hao wawili.

Wabunge wengine wa Kilifi akiwemo Michael Kingi (Magarini), Teddy Mwambire (Ganze), William Kamoti (Rabai) na Ken Chonga (Kilifi Kusini) wanavutia upande wa Bw Kingi na wanaunga mkono mwito wa umoja wa Pwani.

Bw Kingi alisema mpango wake ni kuvileta pamoja vyama vya Kadu Asili, Shirikisho, Umoja Summit na Devolution Party of Kenya (DPK) miongoni mwa vyengine pamoja.

Mpango huu unatazamiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu kulingana na Bw Kingi.

“Tayari tupo kwenye mazungumzo na viongozi tofauti na washikadau. Maongezi hayo yanahusisha viongozi wa vyama hivyo ambavyo vipo tayari Pwani,” akasema.

Hatua hii inatazamiwa kukisambaratisha chama cha ODM ambacho siku za hivi majuzi kilipata pigo katika kaunti ya Kwale kwa kushindwa kunyakua kiti cha Msambweni katika uchaguzi mdogo.

Kushindwa kwenye uchaguzi huo na kuja kwa mwito unaoongozwa na Bw Kingi kunakiweka pabaya chama cha ODM wakati siasa za 2022 zinapopamba moto.

You can share this post!

Chelsea wamtimua kocha Frank Lampard baada ya miezi 18

KOTH BIRO: Gattuso ashindwa kubeba Ruaraka katika fainali