Kingi azidi kubanwa pembeni

Kingi azidi kubanwa pembeni

Na ALEX KALAMA

CHAMA cha Kadu-Asili kimetilia shaka nia ya Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kuleta umoja wa Pwani na hivyo kuzidi kumsukuma gavana huyo pembeni kisiasa.

Chama hicho ni moja kati ya vitano ambavyo vilitarajiwa kuvunjwa ili kuunda chama kimoja cha Pwani, lakini viongozi wao wakakataa wazo hilo na badala yake kusema wataunda muungano wa vyama.

Kiongozi wa Chama cha Kadu-Asili, Bw Gerald Thoya alidai kuwa Bw Kingi alifahamu nafasi yake ya kuwa maarufu kupitia kwa Chama cha ODM ilikuwa inakaribia kuisha kwa vile atakamilisha kipindi chake cha pili cha uongozi mwaka ujao, na hivyo wito wake wa kuunganisha vyama vya Pwani ulilenga kumnufaisha kibinafsi.

Bw Kingi, ambaye wiki iliyopita alipokonywa wadhifa wake wa uenyekiti wa ODM Kilifi, alikuwa mstari wa mbele kupigania umoja wa wanasiasa wa Pwani kuelekea kwa uchaguzi wa 2022.

Hata hivyo, mapema mwaka huu, alilalamikia jinsi viongozi wengine walivyomwacha pweke katika safari hiyo na hivi majuzi ripoti ziliibuka kwamba ameamua kuunda chama kingine kipya.

“Tangu mwaka wa 2007 sisi tulikuwa tunashinikiza Pwani isimame na chama chake, lakini Kingi akaendelea kubaki katika ODM hadi leo. Mwaka wa 2017 tulikejeliwa kwamba vyama vyetu vya Pwani ni magogo matano kwa vile hatukuwa na mgombea urais,” akasema Bw Thoya.

Vyama vingine vya Pwani ambavyo vilitarajiwa kuungana ni Shirikisho, Republican Congress, Umoja Summit na Communist.

Bw Thoya alifafanua kuwa majadiliano yangali yanaendelea kuhusu uundaji wa muungano wa vyama vya Pwani, akikariri kuwa azimio lililotangazwa Voi mnamo Julai 17 lilipelekea kubuniwa kwa kamati ndogo ambayo itawapa mwelekeo kamili baadaye.

“Naamini kwamba tutapata mwelekeo mwafaka na msingi thabiti wa muungano huo na tutafurahi kuwaeleza wananchi mambo haya hivi punde,” akasema.

Wakati huo huo, wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wamedai kuwa ODM huenda ikawa hatarini kupoteza umaarufu Pwani baada ya kumpokonya Bw Kingi uenyekiti Kilifi.

“Kingi ndiye gavana pekee kutoka Pwani ambaye alisaidia chama hicho kupata uungwaji mkono kwa asilimia kubwa hasa kaunti ya Kilifi. Ambapo kiongozi huyo alisaidia ODM kunyakua viti vyote vikubwa vya uongozi kuanzia ugavana,useneta, uwakilishi wa wanawake na hata ubunge, kwa hivyo ameacha pengo kwenye chama hicho,” alisema mchanganuzi wa siasa, Bw Alfred Katana.

Viongozi wa chama hicho katika Kaunti ya Kilifi walimshutumu gavana huyo kwa kumsaliti kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, alipoanza kupigania uundaji wa chama cha Pwani. Bw Odinga alikuwa akipinga uundaji wa chama hicho akisema kitasababisha siasa za ukabila.

Vile vile, Bw Kingi, ambaye amekuwa akikosa kuhudhuria mikutano ya Bw Odinga maeneo ya Pwani kwa muda mrefu sasa, alilaumiwa kwa kutotoa uongozi bora chamani wakati ambapo vyama vingine vinazidi kujitahidi kutafuta umaarufu kwa maandalizi ya uchaguzi ujao.

You can share this post!

Hofu kuhusu waliko watu watatu baada ya boti kusombwa na...

Kituyi apuuzilia mbali mkutano wa Raila na OKA