Kingi, Muturi na Mutua hatarini msajili akikosa kuwatambua

Kingi, Muturi na Mutua hatarini msajili akikosa kuwatambua

NA BENSON MATHEKA

HATIMA ya Gavana wa Machakos Alfred Mutua, mwenzake wa Kilifi Amason Kingi na Spika wa Bunge ya Kitaifa Justin Muturi kwenye uchaguzi mkuu ujao haijulikani, baada ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu, kukataa kutambua vyama vyao kama wanachama wa muungano wa Kenya Kwanza.

Watatu hao wamekuwa wakipigia debe azma ya urais ya Naibu Rais Dkt William Ruto ambaye amekuwa akiwatambua miongoni mwa vinara wa muungano wa Kenya Kwanza.

Dkt Mutua na Bw Kingi waliondoa vyama vyao vya Maendeleo Chap Chap na Pamoja African Alliance (PAA) katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, wakidai mkataba wake haukuwa na uwazi.

Hata hivyo, juhudi zao za kujiondoa katika muungano huo unaoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ziligonga mwamba, Msajili wa Vyama vya Kisiasa aliposisitiza kuwa mkataba wa Azimio umefunga vyama vyao hadi miezi mitatu baada ya uchaguzi mkuu ujao.

TAARIFA

Kwenye taarifa aliyotoa jana, Bi Nderitu alithibitisha kwamba vyama vya Maendeleo Chap Chap, PAA na Democratic Party cha Bw Muturi si wanachama wa muungano wa Kenya Kwanza.

“Msajili wa Vyama vya Kisiasa anatoa arifa kwa umma kwamba vyama 11 vilivyoorodheshwa hapa chini ndivyo wanachama halali wa muungano wa Kenya Kwanza kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Kisiasa, 2011,” ilisema ilani ya Bi Nderitu.

Kulingana na Bi Nderitu, Muungano wa Kenya Kwanza, umeundwa na vyama11 vikiwemo vitatu vilivyouanzisha vya United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto, Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi na Ford Kenya kinachoongozwa na seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Vyama vingine vilivyoongezwa katika muungano huo baada ya kusajiliwa ni Chama Cha Kazi kinachoongozwa na Moses Kuria, Communist Party of Kenya (CPK), Devolution Party of Kenya (DPK) na Economic Freedom Party (EFP).

Vingine ni Farmers Party (FP) cha aliyekuwa katibu wa wizara Irungu Nyakera, The Service Party (TSP) kinachoongozwa na aliyekuwa waziri Mwangi Kiunjuri, Tujibebe Wakenya Party (Jibebe) cha aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo na Umoja na Maendeleo Party.

Dkt Mutua, Bw Kingi na Bw Muturi walitia saini Mkataba wa Maelewano (MOU) na Dkt Ruto kuunga azma yake ya urais naye akaahidi kuwatengea baadhi ya nyadhifa iwapo atashinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 na kuunda serikali.

Hata hivyo, kutotambuliwa kwa vyama vyao na msajili kama wanachama wa muungano wa Kenya Kwanza, kunamaanisha kuwa mkataba wao na Dkt Ruto hautambuliwi kisheria na hawawezi kuchukua hatua yoyote akiamua kuwaruka.

Hatua hii inawaacha kwenye kizungumkuti kwa kuwa Azimio inaweza kukosa kuwachangamkia wakiamua kurudi kwa kile ambacho wachambuzi wa siasa wanataja kama usaliti wao.

“Kisheria, vyama vyao ni sehemu ya Azimio. Lakini kurudi kwao katika muungano huo hakuwezi kuwasaidia kwa kuwa wanachukuliwa kama wasaliti kufuatia ukuruba wao na Dkt Ruto,” akasema mdadisi wa siasa Francis Ambwao.

You can share this post!

Jinsi nidhamu inavyosaidia vijana wa LA FC kupata ufanisi

Wazee waunga azma ya Kibwana kuwania useneta

T L