Kingi ni msaliti, viongozi wadai

Kingi ni msaliti, viongozi wadai

NA WINNIE ATIENO

BAADHI ya viongozi wa pwani wamedai kwamba Gavana wa Kilifi Amason Kingi alisaliti eneo la Pwani kwa kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu wa Rais William Ruto.

Wakiwa katika kampeni za Azimio La Umoja, Gavana Hassan Joho, mwaniaji wa ugavana kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro, Naibu Gavana wa Kilifi Bw Gideon Saburi, Mbunge wa Ganze Bw Teddy Mwambire na mwenzake wa Likoni Bi Mishi Mboko walisema Bw Kingi hajali maslahi ya wakazi wa Pwani.

Bw Joho alisema Gavana Kingi alikosea kuhama chama cha Bw Raila Odinga ambaye alimkuza kisiasa na kujiunga na kile cha mpinzani wake Bw Ruto.

Bw Kingi ambaye anahusishwa na chama cha Pamoja African Alliance alijiunga na muungano wa Azimio La Umoja lakini akauhama na kujiunga na Kenya Kwanza.

Alidai mkataba wa Azimio haukuwa na uwazi.

Lakini Gavana Joho alisema Bw Kingi anapotosha wapwani.

“Afadhali kungekuwa na mpwani mwenzetu ambaye yeye anataka kutoa wapwani na kuwapeleka mahali yeye mwenyewe anasimama. Lakini huwezi kutoa wapwani na kuwapeleka kwa mtu ambaye hana mbele wala nyuma. Unapeleka wapwani kwa mtu ambaye anajulikana kwa mabaya hasa kwa masuala ya mashamba,” alisema Bw Joho.

Alisema ni kinaya kwa Naibu wa Rais kuapa kuwa atamaliza matatizo ya ardhi ilhali anamiliki shamba la ekari 2,536 huko kaunti ya Taita-Taveta, huku mamia ya wakazi wangali maskwota.

Bw Ruto alisema alizawadiwa shamba hilo baada ya kumsaidia aliyekuwa Mbunge wa Taveta Basil Criticos kulipa mkopo aliokuwa akidaiwa na Shirika la Fedha la Kilimo (AFC).

“Kwa nini Bw Criticos akupe shamba, kwani wewe ni mtoto wake ndio upewe shamba hilo lote? Wacha kutudanganya tunakujua, hata shule ya Langata ambapo umejengea hoteli tunajua. Hatujasahau kisa cha marehemu Mzee Gilbert Muteshi,” alisema Bw Saburi.

Bw Joho alisema pwani itanufaika na uongozi wa Bw Odinga tofauti na mpinzani wake Bw Ruto.

Aliwasihi wapwani kumuunga mkono mgombea urais huyo wa Azimio ili waweze kunufaika na kupika jeki azma yake ya kutaka kugombania kiti hicho kwenye uchaguzi wa 2027.

Bw Joho alikuwa anapania kugombania urais uchaguzi wa Agosti 9, lakini alikubali kumuunga mkono Bw Odinga ambaye alimtaja kama babake wa siasa.Hata hivyo, Bw Joho alisema baada ya Bw Odinga, kukamilisha hatamu yake, wapwani watakuwa na nafasi bora ya kugombania kiti hicho.

“Tunamuunga mkono Bw Odinga anifungulie njia nikingojea urais kwa hamu na ghamu. Bw Odinga atakuwa rais wa tano mimi nitakuwa wa sita. Msidanganywe na Naibu wa Rais William Ruto ambaye si mkweli, anawahadaa tu sababu anasaka kura,” alisema Bw Joho.

  • Tags

You can share this post!

Wafalme Ogier na Loeb kunogesha Safari Rally iliyoshuhudia...

KIGODA CHA PWANI: Raila na Ruto kutumia ardhi kama chambo...

T L