MakalaSiasa

KING'ORI: Hii BBI sasa imeanza kuwagawanya Wakenya

February 27th, 2020 2 min read

Na Kinyua Bin King’ori

MIKUTANO inayoendelea nchini ya Jopo la Maridhiano (BBI) inafaa kukomeshwa, kwa maana wanasiasa wameanza kuitumia kupalilia ukabila na chuki.

Wanasiasa wamelemaza malengo ya BBI kuunganisha Wakenya na badala yake inatumiwa kugawanya Wakenya.

Mikutano ya BBI iliyofanyika katika Kaunti za Kisii, Kakamega, Mombasa, Kitui, Garissa na Narok inafaa kutumiwa kutathmini ikiwa kweli BBI itaokoa Kenya kumaliza ukabila, ufisadi, maonevu, vita baada ya kila uchaguzi mkuu, mageuzi katika Tume Huru ya Uchaguzi ni Mipaka (IEBC) na kadhalika.

Kwanza, wanasiasa wameharibu mpango huo kwa kuingiza siasa katika mchakato mzima kwa kupotosha raia kuhusu maswala yaliyomo katika ripoti ya BBI.

Wanatumia mbinu hiyo kwa sababu wanajua raia wengi hawajasoma ripoti hiyo kutokana na jinsi serikali imezembea au kuchelewesha kusambaza nakala za BBI mashinani.?Viongozi wamegeuza BBI kuwa jukwaa la malumbano na kueneza chuki badala ya umoja na maridhiano.

Jopokazi la BBI linaloongozwa na seneta wa Garissa, Yusuf Haji limefeli kwa kukubali wanasiasa kujitwika majukumu ya kutekeleza wajibu kwa niaba yao.

Nasisitiza hivyo kwa maana katika mikutano yote ya BBI anayepokea mapendekezo ya umma ni kiongozi wa upinzani, Raila Odinga?

Kwa maoni yangu, hatua ya kamati ya Haji kukubali mapendekezo kupokelewa na Raila Odinga badala yao wamefeli na shughuli za BBI sasa ni siasa na malumbano tu baina ya wafuasi wa Rais Uhuru, Raila Odinga na Dkt William Ruto.

Shughuli za kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kukumbatia masuala muhimu yaliyomo kwenye BBI zimepuuzwa na kile tunasikia kutoka kwa wanasiasa ni kura ya maamuzi au uchaguzi wa 2022 na kubuniwa kwa vyeo zaidi.

Nauliza, je, Raila anapokea mapendekezo ya umma kama Nani? Je, kwa nini jopokazi husika lisifike kwenye mikutano hiyo kupokea mapendekezo hayo? Je, wananchi wanafaa kutoa maoni yao kwa mikutano au kufika mbele ya jopokazi hilo katika vikao maalum?

Wananchi wafaa kupewa mwelekeo kuhusu njia nzuri ya kuzingatia.?Lengo la BBI si kuwazuia watu fulani kuwa viongozi katika maeneo fulani nchini, bali kuhamasisha umma kuishi kwa kwa umoja, upendo na maridhiano bila kuzingatia kabila, mirengo ya kisiasa au dini.

Lakini ikiwa matamshi kama yaliyotolewa na viongozi katika mkutano wa Narok yatakuwa yakipewa nafasi, basi hata mkutano unaotarajiwa uwanjani Kinoru kesho, Kaunti ya Meru hauna maana yoyote kwa wakazi wa Meru.