Makala

KINGSTAR: Atesa anga kwa vibao vyake 'Nataka Wajue', 'Mapenzi ni Sumu'

May 8th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

NDIO ameanza kupiga ngoma ambapo amepania kukwea milima na mabonde kusudi kutinga levo ya kimataifa katika burudani ya muziki wa kizazi kipya.

Huyu ni Evans Kamau Mbatia ambaye kwa jina la muziki anafahamika kama Kingstar Champion. Kando na muziki Evans amehitimu kwa shahada ya diploma katika masuala ya teknolojia (IT).

Anasema kulingana na jina la Kingstar anataka kuibuka kiongozi wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini.

”Ninaamini kwa juhudi zangu siku moja nitaileta humu nchini tuzo ya msanii bora Afrika Mashariki,” alisema na kuongeza kwamba kwa neema yake Mungu anajikaze kiume kuona ametimiza ndoto zake katika muziki.

Anaorodheshwa kati ya wasanii wa kizazi kipya waliotunga nyimbo zilizotoa mwito kwa Wakenya wapendane kabla ya muafaka wa handishake iliyofanywa baina ya rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Katika nyimbo hiyo nanukuu sehemu ya nyimbo hiyo ‘Wakenya tupendane bila kujali ukabila kwani wote ni mandugu hata kama umetoka sehemu gani ya Kenya.”

Pia anasema ”Ukabila wa nini? Mungu alituumba kuwa jamii moja, lakini shetani ndiye alituingilia na kuanza kuuana.”

Anatoa mwito kwa Wanajeshi kujitolea mhanga kulinda Wakenya dhidi ya Al-shabaab ambao wanawaua Wakenya wakubwa na wadogo bila huruma.

Mwanamuziki huyu anaamini ipo siku ataileta humu nchini tuzo ya msanii bora Afrika Mashariki. Picha/ John Kimwere

Anawashauri usiku wasilale mbali wajitahidi kuweka ulinzi kwa Wakenya viongozi na wananchi wa kawaida.

Anawataka wafahamu kwamba walikula kiapo kwamba watalinda Wakenya wote. Hakika ina maana Mungu alimtumia kutunga nyimbo hiyo kabla ya kuonyesha uhalisia wake ambapo rais alifanya muafaka huo na kiongozi wa upinzani ili Wakenya kudumisha amani.

Katika mpango mzima mwanamuziki huyu amefaulu kutunga nyimbo 15 lakini amerekodi na kutoa fataki nne, audio moja na video tatu.

Tambo za video zikiwa ‘Nataka Wajue,’ ‘Mapenzi ni Sumu,’ na ‘Wakenya tupendane,’ nayo audio ikiwa ‘Ni Moyo.’ Anashukuru maana kati ya nyimbo hizo, fataki ya Nataka wajue imepata mpengo na kuchezwa kupitia KBC Radio Taifa. Kwenye nyimbo hizo amefanya kazi na maprodyuza Willison na Sum G.

”Bila mapendeleo nataka kujitahidi kwa udi na uvumba angalau nifike viwango vya waimbaji mahiri duniani levo ya mwimbaji maarufu wa Bongo Fleva ‘Diamond Platinumz aliyeghani nyimbo kama Sikomi na African Beauty kati ya zingine.

Mwanamuziki huyu ansema gharama ya kurekodi nyimbo ni ghali mno ambapo inadidimiza juhudi za waimbaji wasiona uwezo kifedha. ”Kusema ukweli baadhi yetu tuna vipaji vya kutunga nyimbo nzuri na kali lakini hali hushindikana tunapofika studio,” alisema.

Hapa Kenya anasema hupangawishwa na nyimbo kama ‘Chaguo la moyo,’ na ‘Baby i love you,’ utunzi wake Otile Brown pia mwimbaji Willy Paul kwa kazi zake kama ‘I DO,’ na ‘Njiwa.’

Anatoa mwito kwa waimbaji wanaokuja kuwa makini wanapotunga nyimbo zao hasa kuzingatia maneno matamu pia mawaidha ya kusaidia jamii.

Kadhalika anashauri waimbaji waliotangulia waache ubinafsi mbali wapendane na kuwashika chipukizi mikono ili kuinua sekta ya muziki wa burudani hapa nchini.