Habari

Kinoti abadili kauli kuhusu PEV

November 24th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti amebadili kauli na kukataa madai kuwa afisi yake imeanzisha mchakato wa kufufua upya kesi za ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Kwenye taarifa aliyotoa kwa vyombo vya habari Jumanne, Bw Kinoti amesema hotuba yake Jumatatu, alipokutana na baadhi ya waathiriwa wa ghasia hizo, haikumaanisha kuwa DCI itafungua upya kesi zilizokamilishwa na faili zao kufungwa.

Alisema kile ambacho afisi yake itashughulikia ni malalamishi yaliyoibuliwa na waathiriwa wa fujo hizo kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanaishi kwa amani.

“DCI imepokea malalamishi kutoka kwa umma; watu ambao wanaamini kuwa mali na maisha yao yamo hatarini kutokana na vitisho vinavyoelekezwa dhidi yao. Haya ndiyo mambo ambayo tutachunguza wala sio kesi ambazo zilikamilishwa,” Bw Kinoti akasema.

Akaongeza: “Ningependa kuwahakikishia Wakenya kwamba tutaendelea kutekeleza wajibu wetu wa kuzuia, kudhibiti uwezekano wowote wa kutokea ghasia popote nchini Kenya. Azma yetu kuu ni kulinda maisha na mali ya Wakenya ambao wameingiwa na hofu kufuatia vitisho vilivyoelekezwa kwao.”

Kumekuwa na ripoti kwamba serikali inapanga kufufua kesi kuhusu ghasia hizo za miaka ya 2007/2008 ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuawa na wengine zaidi ya 650,000 wakaachwa bila makao.

Mnamo Jumatatu, Bw Kinoti aliwapokea zaidi ya waathiriwa 120 wa ghasia hizo ambao walifika katika makao makuu ya DCI kuandikisha taarifa kuhusu vitisho ambavyo walidai wamekuwa wakipokea haswa katika maeneo kadha ya Rift Valley.

Baada ya Bw Kinoti kukutana na watu hao, alisema kuwa kesi 72 za mauaji, 144 za kupokonywa ardhi na kesi 118 za vitisho kuhusiana na ghasia ziliandikishwa.

Mkurugenzi huyo wa DCI alisisitiza atafanya kila awezalo kisheria kuwachunguza na kuwakamata wahusika wa ghasia baada ya uchaguzi mkuu wa 2007, akisema hiyo itafanyika “hivi karibuni.”

“Hivi karibuni mtaona matokeo ya shughuli ya leo (jana Jumatatu). Tutawasaka. Najua wanasubiri ghasia zingine za baada ya uchaguzi zifanyike. Wajaribu tena. Tutafuata ukweli; andaeni ushahidi wote na mseme huyu ndiye anamwandama yule au huyu ndiye alimuua fulani,” Bw Kinoti akasema Jumatatu.

Lakini Jumanne, Mkurugenzi huyo wa DCI amesema kwenye taarifa kwamba afisi yake ikipokea malalamishi kutoka mtu yeyote au makundi ya watu, ni wajibu wake kufanya uchunguzi bila mapendeleo.

“Kulingana na matokeo ya uchunguzi, tunaweza kuwafungulia wahusika mashtaka au tufunge faili ikiwa hatutapa ushahidi wa kutosha,” Bw Kinoti akasema.