Habari Mseto

Kinoti afichua Walaghai hujaribu kumhonga kwa mamilioni

December 21st, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Bw George Kinoti ameelezea masaibu yake mikononi mwa wakora ambao hujaribu kumhonga mamilioni ya fedha ili kuelekeza utendakazi wake.

Alisema maafisa wake huandamwa na walaghai wanaotaka kuwahonga kila uchao.

Bw Kinoti alisema kila siku yeye mwenyewe hukumbana na visa vya watu wanaotaka kumhonga mamilioni ya pesa, japo anakataa kutokana na mwito wake wa kuhudumia taifa ipasavyo.

“Ni vigumu zipite saa 24 bila kisa cha mtu kujaribu kunihonga, hii ni hali ya kila siku, ni hali ya maisha nchi hii. Huwa ninapendekezewa pesa nyingi kiasi cha kuweza kuvuruga mtu kichwa na ni mamilioni kwa wakati mmoja,” akasema Bw Kinoti.

Lakini alisema alipoanza kazi hiyo alijua alichoingia ofisini kufanya na ushauri aliopewa na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kupewa kazi.

“Wakati tuliteuliwa pamoja na Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) , tulipewa masharti na maelekezo. Tulishauriwa na Rais na hivyo kila siku tunafuata ushauri wake,” akasema afisa huyo.