Habari Mseto

Kinoti avunjilia mbali kitengo cha Flying Squad

January 1st, 2020 1 min read

Na JOSEPH NDUNDA

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Jinai George Kinoti alivunjilia mbali kitengo cha Flying Squad mnamo Jumanne na kupunguza maafisa wa Kitengo cha Kuzuia Uhalifu Maalum katika kile kinachoonekana kama hatua ya kung’oa maafisa wahuni katika ngazi za DCI.

Wapelelezi katika vitengo hivyo viwili maalum vya DCI wameshutumiwa kwa kutekeleza wizi wa kimabavu pamoja na aina nyingine za uhalifu nchini ambapo Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i mnamo Februari 2018 aliamrisha kitengo cha Flying Squad eneo la Nairobi kuvunjwa kufuatia wimbi la uhalifu Nairobi ambapo kitengo hicho kilielekezewa lawama.

Maafisa hao walihamishwa katika vituo vya polisi kwenye maeneo ya mbali lakini wengi wao waliitwa tena na Kinoti na kuwekwa katika makundi kwenye afisi za DCI eneo la Parklands.

Katika hatua ya mpangilio mpya jana, DCI pia alipunguza SCPU kuwa kitengo kidogo na kuipatia jina jipya la Special Service Unit huku nafasi ya kitengo cha Flying Squad ikitwaliwa na kikosi kipya kilichobuniwa kwa jina Sting Squad Headquarters [SSH] katika makao makuu ya DCI.

Kitengo cha SSU kitakuwa na afisi Nairobi eneo ambapo afisi za SCPU zilikuwa katika makao makuu ya Polisi wa Trafiki Nairobi kwenye barabara ya Ngong.

Maafisa wa Flying Squad na SCPU wamekuwa wakirejelea majukumu na wakati mwingine kufanya majukumu ya maafisa wa SPIV katika Huduma ya Polisi Nchini.

Maafisa wote katika afisi za kimaeneo za kitengo cha Flying Squad na sehemu kubwa ya afisi za SCPU watahamishwa katika afisi mpya zilizobuniwa.

Wakati huo huo, DCI imetangaza nafasi za kazi kwa maafisa wa DCI wanaotaka kujiunga na vitengo hivyo vipya vilivyobuniwa.