Kinoti awaambia wabunge kwamba mwili wa Agnes Wanjiru ulipatikana katika shimo la majitaka

Kinoti awaambia wabunge kwamba mwili wa Agnes Wanjiru ulipatikana katika shimo la majitaka

Na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti, Alhamisi aliwashangaza wabunge alipofichua kuwa mwili wa marehemu Agnes Wanjiru aliyeuawa na wanajeshi wa Uingereza mjini Nanyuki, ulipatikana umetupwa katika shimo la majitaka.

Bw Kinoti alikuwa amefika mbele ya wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni kutoa maelezo kuhusu uchunguzi kuhusu mauaji ya mwanamke huyo yaliyotokea mwaka 2012.

Mkuu huyo wa DCI aliwaambia wanachama wa Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa Mbunge wa Saku Dida Rasso, kuwa uchunguzi kuhusu kifo hicho unaendelea vizuri na kwamba maafisa wanashirikiana na wale wa Uingereza kutanzua kitendawili kuhusu kifo hicho.

“Maafisa wanajiandaa kusafiri hadi Uingereza kuhoji mshukiwa wa mauaji ya Agnes Wanjiru na mashahidi. Tayari majina ya mashahidi yamebainika,” Bw Kinoti akawaambia wanachama wa kamati hiyo katika majengo ya bunge, Nairobi.

Maiti ya Wanjiru ilipatikana miezi miwili baada ya kutoweka usiku mmoja ambapo alikuwa akiburudika katika kilabu kimoja na baadhi ya wanajeshi wa Uingereza.

Hata hivyo, kamati hiyo ililaumu polisi kwa kujivuta katika uchunguzi wa mauaji hayo.

“Tangu 2012 hadi wakati huu, bila shaka huenda mashahidi wengi tayari wamefariki au itakuwa vugumu kuwapata. Swali ni je, mbona uchunguzi wenu umechukua muda mrefu kiasi hiki? Miaka tisa ni muda mrefu zaidi,” akasema Mbunge wa Kinangop Zachary Kwenya.

Mbunge wa Yatta Charles Kilonzo alielekeza kidole cha lawama kwa Bw Kinoti na Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai kwa kuchelewesha uchunguzi kuhusu mauaji hayo.

Alidai hiyo ni njama ya maafisa wa polisi kuhujumu uchunguzi huo na kunyima familia ya marehemu Wanjiru haki.

“Ulikuwa mchunguzi mkuu katika suala hili na hujawahi kupendekeza uchunguzi maalum kuhusu kifo hicho. Nakumbuka kuwa ulikamilisha haraka uchunguzi kuhusu kifo cha aliyekuwa mfanyabiashara raia wa Uholanzi Tob Cohen hadi washukiwa wakakamatwa. Lakini kwa sababu hiki ni kifo cha Mkenya maskini (Bi Wanjiru), uchunguzi huu unacheleweshwa kwa miaka tisa,” akasema Bw Kilonzo.

Wakenya walipokuwa wakilaani kifo hicho, maelezo yaliibuka kuwa wanajeshi wa Uingereza wanaoshukiwa kutekeleza mauaji hayo walitoa mzaha kupitia mtandao wa Facebook kuhusu kisa hicho.

Katika habari zilizochapishwa katika gazeti la Uingereza la “The Times” toleo la Jumapili Oktoba 31, 2021, zilisema kuwa wanajeshi tisa wa Uingereza, akiwemo yule anayeshukiwa kumuua Wanjiru, walitumia maneno ya mzaha wakati mwili ulipatikana Nanyuki.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU

Mshindi wa kwanza wa shindano la Mozzart la Omoka na Moti...

T L