Michezo

Kinyago na Volcano vitani ligi ya KYSD

September 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KAMPENI za kuwania ubingwa wa Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 zinatazamiwa kuendelea kuchacha wikendi hii ambapo mechi sita zimepangwa kuchezwa katika uwanja wa KYSD Kamukunji, Nairobi.

Mabingwa watetezi Kinyago United, Volcano FC, Tico Raiders na Sharp Boys kila moja itakuwa kazini kupigania pointi tatu muhimu ili kuendelea kujiongezea matumaini ya kufanya kweli msimu huu.

Jumapili ijayo chipukizi wa Sharp Boys watakutanishwa na Tico Raiders kwenye patashika inayotazamiwa kushuhudia msisimko mkali.

”Bila kujipigia debe licha ya upinzani mkali unaoshuhudiwa kwenye mechi za muhula huu ninaamini vijana wangu wamekaa pazuri kufanya kweli,” alisema kocha wa Sharp Boys, Boniface Kyalo.

Kinyago ya kocha, Anthony Maina itakuwa kazini kutafuta alama tatu ili kuendelea kukaa kileleni mwa jedwali ya ngarambe hiyo itakapolimana na Pumwani Foundation.

Nahodha wa Kinyago, Samuel Ndonye alisema “Kama ilivyo desturi yetu tangu kampeni za msimu huu zianze hakuna lingine mbali tumepania kuingia mjegoni kwa kusudio moja kutesa wapinzani wetu na kubeba alama zote.”

Kinyago inayolenga kutwaa ubingwa wa taji hilo kwa mara ya 13 inaongoza kwa kufikisha pointi 30 baada ya kushinda mechi kumi ambazo imeshiriki.

Nayo Volcano FC inayofunga mbili bora kwa alama 23 itateremka dimbani kukabili Fearless FC kila moja ikilenga kushusha ubabe wake. Fearless itacheza mchezo huo huku ikijivunia kudhalilisha Fearless Academy kwa magoli 7-1 wiki iliyopita.

Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, Jumamosi Young Achievers itacheza na Locomotive, MASA itaumana na Pro Soccer Academy nayo Pumwani Ajax itamenyana na Fearless Academy.