Michezo

Kinyago na Volcano zatazamiwa kutesa wikendi

September 12th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KINYAGO United na Volcano FC kila moja inapigiwa chapuo kufanya kweli wikendi hii kwenye kampeni za michuano ya Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14.

Mabingwa watetezi, Kinyago United ya kocha, Anthony Maina Jumamosi hii imeratibiwa kucheza na Young Elephant uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi.

Nayo Volcano FC Jumapili itakuwa mbioni kuwinda alama tatu ili kuendelea kujiongezea matumaini ya kufanya kweli itakapokabili Young Achievers.

”Tumepania kujitahidi kwa udi na uvumba kwenye mchezo huo kutafuta alama zote muhimu maana tunafahamu washiriki wote wamejipanga kutubomoa ili kuzima ndoto yetu ya kushinda taji hilo kwa mara ya 13,” alisema nahodha wa Kinyago, Samuel Ndonye.

Kinyago United inaedelea kufanya kweli kwenye kampeni za msimu huu ambapo ingali kifua mbele kwa kufikisha pointi 27 baada ya kusakata mechi tisa na kushinda zote.

Nayo Volcano imetinga mbili bora kwa alama 20, moja mbele ya Fearless FC huku Sharp Boys ikizoa alama 18 na kufunga tatu bora.

Kwenye ratiba ya Jumamosi hii, Pro Soccer Academy itaingia mzigoni kukabili Pumwani Foundation, Lehmans FC itapepetana na Tico Raiders nayo Gravo Legends itatifua vumbi dhidi ya Locomotive FC.

Jumapili, State Rangers italimana na MASA nayo Fearless itakutanishwa na Fearless Academy.