Michezo

Kinyago na Volcano zazidi kuwika

September 15th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

CHIPUKIZI wa Kinyago United na Volcano FC waliendelea kunyorosha wapinzani wao kwenye Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 muhula huu baada ya kila moja kuvuna pointi tatu muhimu.

Kinyago United mabingwa watetezi wa taji hilo chini ya kocha, Anthony Maina ilisajili ushindi wa kumi bila kuteleza ilipochoma Young Elephants kwa magoli 4-0 uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi.

Kinyago inayolenga kushinda taji hilo kwa mara ya 13 iliendelea kukaa kileleni huku Young Achievers ikiteleza na kuangua pua ilipozimwa mabao 3-0 na Volcano FC. Kinyago ilishusha mchezo safi ikipania kuendeleza mtindo wa kugawa dozi mbele ya wapinzani wao.

Vijana hao walizoa ufanisi huo kupitia Samuel Ndonye (nahodha), Thierry Henry, Jahson Wakachala na Austine Okoth waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

Wachezaji wa Locomotive FC wanaoshiriki kinyang’anyiro cha Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14. Picha/ John Kimwere

”Bila kuwapigia debe kamwe sina hofu kuwashukuru wenzangu kwa kazi njema wanaofanya msimu huu,” alisema nahodha huyo wa Kinyago. Nao wafungaji wa Volcano FC inakamata mbili bora kwenye jedwali walikuwa Yahya Farah, Mohamed Juma na Abdirzack Adbullahi waliocheka na nyavu mara moja kila mmoja.

MASA ilituzwa pointi tatu bila jasho ikiwa ni ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao State Rangers kuingia mitini. Nao wachana nyavu Adnan Yusuf na Abdikadar Ahmed kila mmoja alipiga kombora mbili safi na kubeba Gravo Legends FC kuzaba Locomotive mabao 4-1.

Goli la Locomotive FC la kufuta machozi lilijazwa kimiani na Michael Okutoyi. Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Tico Raiders ilitandikwa mabao 4-2 na Lehmans, Fearless FC ililima wenzao wa Fearless Academy magoli 7-1 huku Pumwani Foundation ikilazwa mabao 2-0 na Pro Soccer Academy.