Michezo

Kinyago, Sharps Boys vitani KYSD

October 3rd, 2019 1 min read

NA JOHN KIMWERE

KIVUMBI kikali kinanukia Jumamosi hii Kinyago United itakapoingia mzigoni kukabili Sharp Boys kwenye mechi ya Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 itakayopigiwa uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi.

”Hakika itakuwa mechi ngumu maana wapinzani wetu wanakuja kivingine ingawa wamepoteza patashika moja katika ya 11 walizocheza,” anasema kocha wa Kinyago United, Anthony Maina na kuongeza kuwa katika mpango mzima hawakati masihara mbali wanapania kuendeleza mtindo wa kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wao ili kushinda taji hilo kwa mara ya 13.

Anasema walipata mtihani mgumu dhidi ya Pro Soccer Academy kabla ya kuichapa bao 1-0 baada ya kukosa huduma zake, Thierry Henry ambaye anaorodheshwa kati ya wachezaji wake wazuri.

Hata hivyo alidokeza kuwa kikosi chake kimo imara maana Thierry Henry amepata afueni anapotazamiwa kuchochea wenzake kwenye juhudi za kupigania pointi tatu.

Wachezaji wa Tico Raiders wanaoshiriki kipute cha KYSD. Tico Raiders itacheza na MASA Jumapili hii. Picha/ John Kimwere

Kinyago chini ya nahodha, Samuel Ndonye inaongoza kwenye jedwali la kipute hicho kwa kufikisha pointi 36, nane mbele ya Fearless FC baada ya kila moja kucheza mechi 12. Nayo Sharp Boys ya kocha, Boniface Kyalo inafunga tatu bora kwa alama 24 kutokana na mechi 11.

Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, Jumamosi hii Pumwani Foundation itaumana na Gravo Legends, Pumwani Ajax itapepetana na Volcano ya nne kwenye jedwali. Young Achievers itavaana na Fearless FC.

Jumapili MASA inayokamata tano bora kwa alama 22, moja mbele ya Lehmans italimana na Tico Raiders, Fearless Academy itakuwa na kibarua kigumu itakapochuana na Locomotive FC. Nayo Young Elephants itagaragazana na Pro Soccer Academy huku Lehmans ikitifua vumbi dhidi ya State Rangers.