Michezo

Kinyago United bado moto licha ya kupigwa breki

February 25th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kinyago United imedhihirisha ingali moto wa kuotea mbali baada ya kuhifadhi taji la Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 licha ya kutoka sare ya bao 1-1 na Fearl kwenye mechi ya tamati iliyosakatiwa uwanjani KYSD, Shaurimoyo Nairobi.

Kinyago United ambayo hunolewa na kocha, Anthony Maina imehifadhi taji hilo kwa mara ya 12 mfululizo ambapo imeketi mkao wa subira kuvishwa ufalme huo baada ya kuibuka kidedea kwa alama 57, tatu mbele ya mahasimu wao MASA baada ya kuteleza na kukandamizwa mabao 3-0 na Volcano FC.

Mechi za kipute cha msimu wa 2018/2019 zilikamilika wikendi ambapo ni makala ya 19 tangu kianzishwe mwaka 2000. ”Sina shaka kupongeza wachezaji wangu hakika walifanya kweli licha ya kwamba walifungua kampeni za vibaya walipodondosha mchuano wa ufunguzi,” alisema kocha Anthony Maina na kuongeza kuwa baadaye walilazimika kutumia maarifa zaidi kukabili wapinzani wao kwenye ngarambe hiyo iliyoshuhudia msisimko wa kipekee msimu huo.

Kinyago United chini ya nahodha, Samuel Ndonye ilitwaa bao hilo kupitia juhudi zake Abubakar Maina nayo Fearl ya kocha, Jonah Makau ilisawazishiwa na Maxwell Mwangi.

Nayo Fernabache ambayo tangu mwanzo ililikuwa inapigiwa chapuo kubeba taji hilo ilimaliza tatu bora kwa kuzoa alama 51 ilipoteleza na kukubali kukiri kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Locomotive FC.

Lenock Abraham na Enock Ochieng alitikisa nyavu mara moja kila mmoja na kusaidia Locomotive kutia kapuni alama tatu naye Aaron Suleiman alitingia Fernabache bao la kufuta machozi.

Kocha Anthony Maina aliye mwanzishi wa KYSD alisema ”Baada ya kukamilisha mechi za ligi sasa vijana wanajiandaa kushiriki kampeni za TOP 8 kwa timu zilizoibuka nane bora.” Ngarambe ya TOP 8 itajumuisha Kinyago United, MASA, Fearl FC, Locomotive, Young Achievers, Sharp Boys, Fernabache ma Volcano FC.

Michuano ya KYSD huandaliwa ili kuendeleza mpango wa kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi mashinani.

”Ligi ya KYSD imefaulu kunoa makucha ya chipukizi wengi ambao baadhi yao tayari huchezea klabu za Ligi Kuu ya Sportpesa pia timu ya taifa ya Harambee Stars kwa wasiozidi umri wa miaka 17,” Ombona alisema na kusisitiza kwamba ingawa ligi hiyo haijapata mdhamini wengi wametambua umuhimu wake. Kati ya chipukizi wa Harambee Stars (U-17) waliotokea Kinyago United ni kama: Brian Opiyo na Bixente Otieno (MASA), Saidi Musa (Star Soccer Academy), Keith Imbali (Kinyago United) ambaye huchezea Gor Mahia Youth.

Ligi hiyo ilijumuisha Kinyago United, Blue Boys, Lehmans, MacMillan, Young Elephants, Locomotive, Fearl, Volcano, Sharp Boys, Young Achievers, Fernabache na MASA.