Michezo

Kinyago United na MASA zang'ang'ania ubingwa KYSD

February 20th, 2019 1 min read

NA JOHN KIMWERE 

TIMU za Kinyago United na MASA zimepiga hatua kwenye mbio za Ligi ya KYSD kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 14 baada ya kuzoa alama tatu na sita mtawalia.

Kinyago United iliicharaza Young Elephants mabao 3-1 na kujiweka pazuri kuhifadhi taji hilo kwa mara ya 12 mfululizo huku MASA ikilaza Sharp Boys mabao 3-0 kisha kutuzwa ushindi wa mezani dhidi ya MacMillan.

”Lazima tushinde mechi ya mwisho maana tukiteleza tu tutakuta mwana siyo wetu,” alisema kocha wa Kinyago United, Anthony Maina.

Kwenye jedwali Kinyago United inakamata usukani kwa kuvuna pointi 56, mbili mbele ya MASA kila moja ikiwa imebakisha mchezo mmoja.

”Wachezaji wangu lazima wajitahidi washinde taji hilo maana wakibeba tu wameahidiwa kufadhili ziara ya kutalii Kaunti ya Mombasa,” alisema na kudai kuwa wameapa kupigana kufa na kupona.

Kwenye patashika hiyo, nahodha Samuel Ndonye wa Kinyago United alitikisa nyavu mara mbili huku Jahson Wakachala akipiga moja safi. Naye John Kimweu aliifungia Y.Elephants.

Kwenye mechi hizo, Young Achievers iliona giza ilipozabwa mabao 3-1 na Lehmans, naye Wesley Obure alicheka na nyavu mara moja na kubeba Fernabache kuzima Blue Boys bao 1-0.

Nayo Fearl ililazimishwa kutoka nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Volcano FC.