Michezo

Kinyago United wanavyonoa makali

April 26th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kinyago United inazidi kudhihirisha kwamba inatosha mboga kutifua kivumbi kikali baada ya kuhifadhi taji la Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 muhula wa 2019/2020.

Kikosi hicho ambacho hutiwa makali na kocha, Anthony Maina kimehifadhi ubingwa wa ngarambe hiyo kwa mara ya 13 mfululizo.

Kinyago United inaendelea kuonyesha ingali moto wa kuotea mbali kwenye kampeni hizo ambapo imetawazwa mafahali wa kipute hicho baada ya kumaliza kidedea kwa kukusanya pointi 83.

Michuano ya msimu wa 2019/2020 ilishuhudia upinzani wa kufa mtu ambapo Fearless FC ya kocha, Jonah Makau ilimaliza ya pili kwa kufikisha alama 73 kwenye jedwali.

Nao wavulana wa Gravo Legends walipigana kwa udi na uvumba na kufunga tatu bora kwa kuvuna pointi 60, mbili mbele ya Sharp Boys.

Mechi za kipute cha muhula huo zilikuwa za makala ya 20 tangu kianzishwe mwaka 2000.

”Nashukuru chipukizi wangu kwa kuhifadhi taji hilo kwa mara nyingine licha ya kupata upinzani mkali mbele ya wapinzani wetu,” kocha huyo amesema na kuongeza kuwa bado wamepania kuweka mikakati yao kabambe kwenye jitihada za kuanza kupigania taji hilo msimu mpya baada ya shughuli za michezo nchini kurejea kawaida.

Inafahamika serikali ilisitisha shughuli zote kote nchini ikiwamo michezo wiki tatu zilizopita ili kuzuia maambukizi ya virusi hatari vya korona.

Tico Raiders pia iliyoshiriki kipute hicho.

”Sina shaka kupongeza wachezaji wangu kwa kazi waliofanya kwenye kampeni za msimu huo ambapo kwa mara ya kwanza wamaliza kati ya nafasi mbili bora,” alisema kocha wa Fearless na kuongeza kuwa muhula huo timu zote zilishusha soka la kujituma kuliko mihula iliyopita.

Hata hivyo, Kinyago United ilijikuta njiapanda kwenye mechi za kuwania taji la TOP 8 iliponyukwa mabao 2-0 na Sharp Boys kwenye nusu fainali iliyoshuhudia ushindani wa kufa mtu.

Michuano ya KYSD huandaliwa kwenye juhudi za kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi mashinani. ”Ligi ya KYSD imenoa wachezaji wengi tu ambao baadhi yao tayari huchezea klabu za Ligi Kuu ya KPL pia timu ya taifa ya Harambee Stars kwa wasiozidi umri wa miaka 17,” Maina alisema na kusisitiza kuwa ingawa ligi hiyo haijapata mdhamini wengi wametambua umuhimu wake.

Baadhi ya wachezaji wa Lemans F.A.

Kati ya chipukizi wa Harambee Stars (U-17) waliotokea Kinyago United ni kama: Brian Opiyo na Bixente Otieno (MASA), Saidi Musa (Star Soccer Academy), Keith Imbali (Kinyago United) ambaye huchezea Gor Mahia Youth.

Ligi hiyo ilijumuisha Kinyago United, Fearless FC, Gravo Legends, Sharp Boys, Lemans F.A, MASA, Volcano FC, Tico Raiders, Young Elephant, Pumwani Ajax, Young Achievers, State Rangers, Pro Soccer Foundation, Locomotive FC, Fearless Academy na Pumwani Foundation.