Michezo

Kinyago United watua kileleni KYSD

August 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

THIERRY HENRY ametikisa wavu mara moja na kubeba Kinyago United kuibandua Volcano FC kileleni mwa Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 baada ya kuilaza goli 1-0 uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi.

Nayo Sharp Boys iliendelea kutesa ilipozaba Gravo Legends kwa magoli 3-2 kwenye mechi iliyoshuhudia msisimko wa kufa mtu.

”Dah! Kampeni za muhula huu hakuna mteremko tulipata ushindi huo kwa jasho dhidi ya wapinzani wetu waliokuwa kifua mbele,” nahodha wa Kinyago Samuel Ndonye alisema huku akipongeza wenzake kwa kujitahidi kiume na kuhakikisha wametwaa ufanisi wa pointi tatu muhimu.

Katika msimamo wa kipute hicho, Kinyago United inaongoza kwa alama 15, mbili mbele ya Sharp Boys sawa na Volcano tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Sharp Boys ilizoa ushindi huo kupitia Victor Aguya aliyepiga kombora mbili safi huku Victor Mugambi akiitingia bao moja. Nao Khalid Mohamed na Hamza Abdirahmah kila mmoja alifungia Gravo Legends goli moja.

Kwenye mfululizo wa matokeo ya mechi hizo, Fearl FC ilituzwa pointi tatu bila jasho ukiwa ni ushindi wa mezani baada ya Pro Soccer kuingia mitini.

State Rangers FC ilitoka nguvu sawa magoli 2-2 na Pumwani Ajax, Fearless Academy ilicharazwa mabao 3-0 na Tico Raiders, Pumwani Foundation ilichapwa magoli 4-1 na Young Achievers huku MASA ikitia kapuni mabao 2-0 mbele ya Young Elephants.

Kinyago United ambayo hutiwa makali na kocha, Anthony Maina ndiyo mabingwa watetezi wa kipute hicho inkolenga kuhifadhi kwa mara ya 13. Hata hivyo inaonekana haitakuwa rahisi maana wapinzani wengine ikiwamo Sharp Boys na Volcano kati ya zingine zinakuja kwa kasi.