Michezo

Kinyago United yaapa kutotishwa kutetea taji

July 16th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kinyago United imepania kujituma kwa udi na uvumba kwenye kampeni za kufukuzia ubingwa wa Ligi ya KYSD (2019/2020) kwa wasiozidi umri wa miaka 14 kwa mara ya 13. Kikosi hicho ambacho hutiwa makali na kocha, Anthony Maina kinalenga kuzua ushindani mkali kutetea taji hilo kilichotwaa msimu uliyopita kwa kuzoa alama 57, tatu mbele ya MASA.

Nayo Fernabache iliyokuwa ikipigiwa chapuo kutwaa taji hilo ilimaliza tatu bora kwa kuzoa alama 51 ilipoteleza na kukubali kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Locomotive FC kwenye mchezo wa mwisho.

Vile vile Kinyago United ilijivunia kutawazwa mabingwa wa timu zilizomaliza kati ya nane bora (Top Eight) msimu uliyopita. Mechi za msimu huu zitakuwa za makala ya 20 tangia ngarambe hiyo ianzishwe mwaka 2000.

Hata hivyo kampeni za msimu huu huenda hazitakuwa rahisi kabisa baada ya washiriki kuonyesha upinzani mkali kwenye mechi za Pre-Season Cup zilizochezwa wiki iliyopita katika Uwanja wa KYSD.

Kwenye michuano hiyo MASA ilitwaa taji hilo baada ya kulemea Kinyago United kwa bao 1-0 katika fainali. Kocha wa Kinyago United amekiri kwamba kampeni za msimu huu kamwe hazitakuwa mteremko maana timu zote zimeonekana zimejipanga vilivyo kuwabomoa na kuwapokonya kombe hilo ambalo wameshinda mara 12.

”Nakumbuka msimu uliyopita tulianza mechi zetu vibaya maana karibu tushindwe kuhifadhi taji hilo, kwa hilo msimu huu tumepania kuwahi mapema mapema ili kujiweka pazuri kuhifadhi kombe na kulishinda kwa mara ya 13,” kocha Anthony Maina alisema na kuongeza kwamba lazima wachezaji wangu wajikaze na kujituma kisabuni maana wanakabiliwa na ushindani wa kufa mtu msimu huu.

Wiki iliyopita kocha wa Sharp Boys, Bonface Kyalo alinukiwa akisema “Michezo ya msimu huu itakuwa ngumu zaidi ambapo upinzani mkali unatazamiwa kushuhudiwa baina ya Kinyago United, MASA na Sharp Boys.” Mechi za KYSD huandaliwa kila mwaka ili kuendeleza mpango wa kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi mashinani.

Ligi ya KYSD inajivunia kunoa makucha ya chipukizi wengi ambao baadhi yao wamefanikiwa kuteuliwa kuchezea klabu za Ligi Kuu ya KPL kati ya zingine nchini pia timu ya Harambee Stars kwa wasiozidi umri wa miaka 17.

Kinyago United inajumuisha wachezaji kama: Peter Gathuri, Newton Maina, Alvin Muteti, Abednego Wawire, Abdallah Shame, Alphonse Ndungu, Thierry Henry, Boniface Ariemba na Samuel Ndonye (nahodha). Pia wapo Jahason Wakachala, Austine Okoth, Iphrahim Oyando, Samuel Kamau, Chrisphine Mamwacha, Titus Muimi, Peter Waweru, Collins Juma na Daniel Mwangi.

Timu 16 zitashiriki kipute cha msimu mpya 2019/2020 ambazo ni:Kinyago United, MASA, Sharp Boys, Young Elephant, Locomotive, Blue Boys, Young Achievers, State Rangers, Black Jack, Gravo Legends, Lehmans, Volcano, Fearless, Spartans, Fernabache na Pumwani Ajax.