Michezo

Kinyago United yalipua State Rangers 7-1

August 5th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Volcano na Kinyago United kila moja iliandikisha pointi tatu muhimu na kutua kati ya nafasi mbili bora kwenye mechi za kuwania Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 msimu huu.

Mabingwa watetezi, Kinyago United ya kocha, Anthony Maina ilirukia mbili bora ilipodhalilisha State Rangers kwa magoli 7-1 kwenye patashika iliyosakatiwa uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi. Nayo Volcano ilitolewa kijasho kikali kabla ya kuzoa ufanisi wa mwepesi wa magoli 3-2 mbele ya Gravo Legends.

Nahodha wa Kinyago, Samuel Ndonye aliongoza wenzake kutesa wapinzani wao baada ya kuhaidi kucheza kila mechi kama fainali maana kipute cha msimu huu kinapigiwa upatu kushuhudia ushindani wa kusisimua.

Kinyago ilipata ufanisi huo kupitia Thierry Henry na Abednego Wawire waliopiga kombora mbili safi kila mmoja huku Boniface Ariemba, Austine Okoth na Jahson Wakachala kila mmoja akiitingia bao moja. Magoli ya State Rangers yalifunikwa kimiani na Idarus Ali.

”Tumepania kuendeleza mtindo huo dhidi ya wapinzani ili kujiweka pazuri kushinda taji hilo kwa mara ya 13,” nahodha huyo wa Kinyago alisema na kuongeza kuwa wanafahamu shughuli siyo mteremko raundi hii. Nao Gravo Legends walitangulia kupata mabao hayo kupitia Adnan Yusuf kabla ya Yahya Farah, Abdirasak Abdullahi na Abdi Jabar kucheka na wavu mara moja kila mmoja na kuzima ndoto ya wenyeji wao.

Kufuatia matokeo hayo, Volcano imetua kileleni mwa kipute hicho kwa kuzoa alama kumi, moja mbele ya Kinyago United baada ya kupiga mechi nne na tatu mtawalia.

Kwenye mechi hizo, Lemans FC ilikung’utwa magoli 7-1 na MASA, Locomotive ilituzwa pointi tatu bila jasho ikiwa ni ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao Pumwani Foundation kuingia mitini.

Nao wavulana wa Sharp Boys waliteleza na kutoka sare ya goli 1-1 dhidi ya Fearless, Tico Raiders ililaza Young Elephant bao 1-0 nazo Fearless Academy na Young Achievers kila moja ilinasa matokeo ya goli 1-1 mbele ya Pro Soccer Academy na Pumwani Ajax mtawalia.