Michezo

Kinyago United yatolewa jasho kisha kulimwa

July 16th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KINYAGO United ilitolewa kijasho kikali kabla ya kuishinda Young Achievers bao 1-0 kwenye utangulizi wa mechi za Ligi ya KYSD 2019/2020 kwa wasiozidi umri wa miaka14 Uwanjani KYSD, Shauri Moyo Nairobi.

Kinyago United inayolenga kutwaa taji hilo kwa mara ya 13 ilipigana kufa na kupona kabla ya Henry Thierry kuitingia bao hilo kipindi cha pili.

Nayo Sharp Boys iliiponda Lemans kwa mabao 2-0 huku Fearless Academy ikilaza Locomotive mabao 3-0 kabla ya kuteleza na kuchomwa kwa mabao 3-1 na Pumwani Foundation.

”Kusema kweli kampeni za msimu huu zimekunjua jamvi kwa kasi,” kocha wa Kinyago United, Anthony Maina alisema na kuongeza kuwa timu zote zimeonyesha zimejipanga kupigania taji hilo kwa nguvu zote.

Sharp Boys ilijipatia ufanisi huo baada ya Boniface Oluoch na Ramadhan Mohammed kila mmoja kufuma kimiani bao moja. Nao wafungaji wa Fearless Academy walikuwa Kevin Musyoki, Rodney Okinyi, Jamaine Kamati na Onesmus Mutheri.

Nao chipukizi wa Pumwani Ajax walibebeshwa kapu la magoli 7-1 na MASA kati ya vikosi vinavyopigiwa chapuo kuibuka moto wa kuotea mbali msimu huu.

Nazo State Rangers na Gravo Legends kila moja iliachia pointi tatu muhimu baada ya kukubali kulala kwa mabao 2-1 na 1-0 mbele ya Young Elephant na Pro Soccer Foundation mtawalia.