Michezo

Kinyago yatetemesha, Volcano yajikwaa KYSD

September 22nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KINYAGO United iliendelea kutesa wapinzani wengine kwenye kampeni za Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 huku Volcano FC ikiteleza na kulala kwa magoli 3-2 mbele ya Fearless FC katika uwanja wa KYSD Kamukunji, Nairobi.

Kinyago United ya kocha, Anthony Maina ilisajili ushindi wa mechi ya 11 muhula huu ilipochoma Pumwani Foundation magoli 4-1.

Vijana hao chini nahodha, Samuel ndonye waliteremka dimbani kufanya kweli na kuhakikisha wamebeba pointi zote muhimu. Walitandaza soka safi na kunasa ufanisi huo kupitia Thierry Henry aliyepiga ‘hat trick’ naye Samuel Ndonye alitinga goli moja.

Kocha wa MASA, Eugene Wethuli akiongea na wachezaji wake kabla ya kushuka dimbani kukabili Pro Soccer Academy kwenye mechi za Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14, uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi. MASA ilishinda magoli 4-0. Picha/ John Kimwere

”Tumejaa furaha tele pia tunashukuru maana tunazidi kuwabwaga wapinzani wetu kwenye kampeni za msimu huu,” alisema kocha wa Kinyago na kuongeza kuwa hawana la ziada mbali wamepania kuendeleza ubabe huo ili kuhakikisha wameshinda taji hilo kwa mara ya 13.

Hata hivyo alionya wachezaji wake kuwa furaha ya ufanisi wao isiwaponde kwenye mechi sijazo. Kadhalika aliwaambia kawaida anataka wakazane kwa udi na uvumba wahifadhi kombe hilo.

Nao chipukizi wa MASA walichapa Pro Soccer Academy magoli 4-0 kupitia Glen Otieno, Finus Otieno, Ashley Konivya na Washington Romero baada ya kila mmoja kutikisa nyavu mara moja.

Kocha wa State Rangers, Boniface Kyalo akizungumza na wachezaji wake. State Rangers ni kati ya timu 16 zinazoshiriki kampeni za Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14. Picha/ John Kimwere

Naye Victor Mugambi alipiga kombora moja safi na kubeba Sharp Boys kuandikisha ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Tico Raiders, Locomotive FC ililimwa mabao 2-1 na Young Achievers yaliyofumwa kimiani na Idris Mwangi. Naye Mark Otieno aliifungia Locomotive bao la kufuta machozi.

Kwenye matokeo hayo, Pumwani Ajax na Fearless Academy kila moja ilizoa alama moja baada ya kutoka sare ya bao 1-1. Nayo chipukizi wa Young Elephants walijikuta kwenye wakati mgumu walipodhalilishwa kwa magoli 5-2 na Lehmans.

Matokeo hayo yamefanya Kinyago United kuendelea kukaa kileleni kwenye jedwali ya kipute hicho kwa kufikisha alama 33 baada ya kushinda mechi zote 11 ambazo imeshiriki.