Michezo

Kinyago yazikaranga MASA na Fearless bila uoga

September 2nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya chipukizi ya Kinyago United ilizigeuza MASA na Fearless kuwa kitoweo ilipoziponda kwa mabao 4-0 na 3-0 mtawalia kwenye patashika za Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 uwanjani KYSD Kamukunji Nairobi.

Mabingwa watetezi, Kinyago inayolenga kushinda ubingwa huo kwa mara ya 13 ilionyesha mechi safi na kuchangia wapinzani wao kukosa maarifa na kila mja kudondosha pointi tatu muhimu. Chini ya nahodha, Samuel Ndonye Kinyago ilibeba mafanikio kupitia juhudi zake Henry Thierry aliyepiga ‘Hat trick,’ nao Peter Irungu na Abednego Wawire kila mmoja aliifungia goli moja.

Nahodha Samuel Ndonye aliongoza chipukizi kuvuna ufanisi kupitia Henry Thierry aliyepiga ‘Hat trick’, nao Peter Irungu na Abednego Wawire kila mmoja aliwatingia goli moja.

”Tunalenga kuendeleza mtindo huo kwenye mechi sijazo ili tuzidi kujiongezea tumaini la kuwabwaga mahasimu wetu ambao wameonekana kuja kwa kasi muhula huu,” alisema kocha wa Kinyago, Anthony Maina.

Naye Victor Aguya alicheka na wavu mara tatu huku Steve Mugambi akipiga kombora moja safi na kubeba Sharp Boys kuchapa Fearless Academy mabao 4-0. Kwenye jedwali ya kipute hicho, Kinyago inaongoza kwa kufikisha alama 24 nayo Sharp Boys imekamata mbili bora kwa alama 17, sawa na sawa na Volcano tofauti ikiwa idadi ya magoli.

Shuti iliyojazwa kimiani na Yakub Farah dakika ya tano lilisaidia Volcano kubeba goli 1-0 dhidi ya Lehmans. State Rangers ilituzwa pointi tatu bila jasho ushindi wa mezani baada ya Pro Soccer kusepa kwa kuiogopea.

Matokeo mengine, Pumwani Ajax iliumwa mabao 3-0 na Young Elephants, Tico Raiders ililaza Locomotive mabao 3-0, Fearless ililima Pumwani Foundation mabao 2-0 naye Young Achievers ilisalimu amri ilipobugizwa mabao 3-0 na Gravo Legends.