KINYUA BIN KING’ORI: Chebukati ashamaliza kazi yake, wasioridhika waende mahakamani

KINYUA BIN KING’ORI: Chebukati ashamaliza kazi yake, wasioridhika waende mahakamani

NA KINYUA BIN KING’ORI

HATIMAYE Dkt WIlliam Ruto aliyegombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita chini ya muungano wa Kenya Kwanza hivi majuzi alitangazwa Rais mteule na kutamatisha kipindi kirefu cha kampeni.

Baada ya maafisa wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujitokeza wazi na kuelezea kujitenga na matokeo ya urais, Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alitekeleza wajibu wake kama msimamizi wa uchaguzi wa urais kwa kutangaza William Ruto raiis mteule wa Kenya Kwa kuzoa kura 7,176,141 dhidi ya kura 6,924,930 za mpinzani wake wa karibu Raila Odinga.

Dkt Ruto alipata asilimia 50.49 na zaidi asilimia 25 ya kura katika kaunti 39 huku Raila akipata asilimia 48.85 na asilimia sawa katika kaunti 35.

Hivyo basi, Wakenya wameamua Dkt William Ruto ndiye atakuwa rais wao katika kipindi cha 2022-2027 na mpira umetupwa miguuni mwake kuthibitisha kweli alistahiki kupewa wadhifa huo wa juu serikalini.

La mno ni raia kuelewa walimaliza kazi yao debeni, Chebukati naye alimaliza kazi yake na uamuzi sasa ni wanasiasa ambao hawajaridhika kuwasilisha kesi na ushahidi wao katika mahakama kupinga matokeo hayo.

Itakuwa busara mno kwa viongozi kutumia njia halali kuelezea kutoridhika kwao bila kutatiza usalama na kuvuruga amani na utulivu nchini.

Nashauri viongozi wote na wananchi kwa jumla kushirikiana na serikali mpya itakayoundwa na Rais mpya Dkt William Ruto bila kujali ikiwa walimpinga au kumuunga mkono ili kumwezesha kuwa na urahisi wa kutekeleza ahadi alizotoa kipindi cha kampeni.

Lazima tukubali japo wawaniaji urais walikuwa wanne, lakini mshindi ni mmoja tu.

Hivyo, tunafaa kujua umuhimu wa kukubali matokeo na kusonga mbele bila kuzua fujo wala kueneza chuki.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: ODM ijipige msasa ndipo iweze kuendelea...

NDIVYO SIVYO: Kauli ‘uchumi umepanda’ haina mashiko na...

T L