KINYUA BIN KING’ORI: Hongera Uhuru na Raila kukubali uamuzi wa mahakama

Na KINYUA BIN KING’ORI

INATIA moyo kuona Wakenya wengi wakiwemo viongozi wa kisiasa wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga ambao ndio waasisi wa mswada wa maridhiano wa BBI uliotupiliwa mbali na Mahakama ya Rufaa wiki iliyopita wakiungana kukumbatia uamuzi huo, japo mchungu kwao kisiasa.

Raila kwa mara ya kwanza amekuwa kiongozi wa kwanza hata kabla ya korti kutoa uamuzi wake kutangaza atakubali uamuzi wowote ule, na kweli baada ya BBI kuzimwa alikubali uamuzi huo.

Hatua ya viongozi hao inafaa kupongezwa maana imeonyesha ukomavu katika kuheshimu idara nyingine kama mahakama, wakati mwingi hasa katika utawala wa Jubilee viongozi wa serikali wamekuwa wakitishia uhuru wa korti zetu kwa kuwatolea vitisho, majaji kuhangaishwa na maamuzi yao mengi kupuuzwa.

Majaji wa mahakama kuu sawia wa Mahakama ya Rufaa waliokuwa wakisikiliza kesi ya BBI nawapa heko sufufu kwa kuonyesha Kenya na dunia umuhimu wa viongozi kuzingatia katiba waliyoapa kuilinda.

Ama kwa hakika nyinyi ni mashujaa katika kutekeleza wajibu wenu.

Kuna wale ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa majaji hao, na huenda watakosa kushangilia uamuzi huo lakini ukweli utabakia mahakama tu ndiyo imetwikwa wajibu wa kutetea katiba na kuhakikisha inazingatiwa bila kuvurugwa na wananchi wa kawaida au viongozi serikalini au vigogo wa kisiasa nchini.

Hayo ndiyo mafanikio makubwa ya Katiba ya 2010 na uamuzi huo umethibitisha katiba yetu imejilinda na imelinda Wakenya na asasi zote serikalini kiasi cha kila idara kutoa maamuzi yao bila kutishiwa au kuhangaishwa na idara nyingine au ikulu ya Rais.

Uamuzi huo umechochea Wakenya kujenga matumaini na imani mpya kwa mahakama zetu. Ukweli huo ni ushindi mkubwa kwa uhuru wa mahakama, ushindi kwa katiba na ukombozi kwa Wanjiku kiasi cha kusadiki anaweza kupata haki kortini bila hofu ya kunyimwa haki kwa sababu moja au nyingine inayokiuka haki zake.

Kwa kuwa BBI imezimwa, sasa inafaa viongozi wote wa kisiasa kukomeshwa malumbano yao kuhusu suala hilo. Haipendezi kuona baadhi yao wakijipiga kifua au wengine kusinyika kutokana na uamuzi huo.

Malumbano yao sasa hayapaswi kuendelea maana yanatishia mipango ya maendeleo, kufifisha juhudi za kufufua uchumi na kuyumbisha hatua za kuhakikisha wakenya wote wamepata chanjo kukabili janga la covid 19.

Ukweli ni kwamba hakuna mshindi wala mshinde katika uamuzi huo bali sote tu washindi na ikawa ni Ushinde basi ni sisi tu washinde.

Kuna mambo mazuri mno yaliyokuwa katika mswada wa BBI, kama vile kuongeza fedha katika serikali za kaunti hadi asilimia 35, kutenga hazina ya vijana, kuwaunganisha Wakenya kwa kuwa na serikali inayojumuisha makabila yote ni maswala muhimu na hayafai kuachwa yazikwe pamoja na BBI.

Kwa vile tunatambua changamoto ambazo zilitatiza tuzifikie mafanikio hayo, viongozi wote wawnaweza kushirikiana bila vitisho kuhakikisha Sheria zimepitishwa Bungeni kutuwezesha kupata mafanikio hayo.

Maelfu ya wakenya mashambani na mijini hawajui Kwa nini wabunge washinde kutekeleza majukumu yao ya kuibuka na sheria zinazomjali Mwananchi wa kawaida anayeteseka Kwa kukosa maendeleo faafu.

Kabla ya Bunge la kumi na moja kumaliza muhula wake na kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 serikali Kwa kushirikisha wabunge inafaa kuhakikisha wameweza kubadilsha baadhi ya sheria ambazo zitahakikisha mashinani Mwananchi amenufaika hata bila BBI.

Kufaulisha kutungwa Kwa Sheria inatakayowezesha kaunti 47 kupokea mgao wa asilimia 35 kutoka wizara ya fedha serikali ya kitaifa itakuwa ushindi Kwa ugatuzi.

Itakuwa hatua kubwa Katika juhudi za kuzidisha Miradi ya Maana mashinani ziteandelea kuzaa matunda.

Tukifanikisha hayo machache kwa sasa, baada ya uchaguzi wa 2022, Serikali itakayochaguliwa itafufua upya juhudi za kubadilisha katiba kwa kuwashirikisha Wakenya wote ila kwa kuzingatia sheria wala sio vitisho.

Mabadiliko ya katiba iwe leo, kesho au baada ya 2022 yanafaa yawe yenye kumfaa mwananchi wala sio kuongeza nyadhifa za uongozi kuwafaidi wanasiasa wachache.

Habari zinazohusiana na hii