KINYUA BIN KING’ORI: Kinga ya corona katika matatu sasa ni wewe na mimi!

Na KINYUA BIN KING’ORI

HATA ingawa wenye matatu wamefurahia hatua ya serikali kuwaruhusu kuanza kubeba abiria kwa asilimia mia moja kuanzia Agosti 9, 2021, wananchi tunaotumia usafiri wa umma sasa tumetwikwa wajibu wa kuamua hatima ya maisha yetu.

Yaani, itategemea jinsi umma utakavyojitolea kujilinda watu wakiwa wanasafiri dhidi ya janga la Covid 19.

Kwanza, tuelewe kuwa hatua hii iliyochukuliwa na Wizara ya Uchukuzi kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ililenga kuokoa sekta ya matatu na kufufua uchumi wa taifa wala haimaanishi kwamba maambukizi ya corona yamepungua.

Serikali ilitambua kuwa wamiliki wa magari ya abiria yakiwemo mabasi ya masafa marefu wameumia mno kutokana na agizo lililowazuia kujaza abiria katika juhudi za kuzuia msambao wa janga la Covid 19 kiasi cha baadhi yao kufilisika huku wengine wakishindwa kulipa madeni yao.

Baadhi yao mali zao zilipigwa mnada na mashirika ya mikopo baada ya kulemewa kwa biashara zao kutatizika na kukosa pesa za kulipia mikopo.

Hata serikali ilipata hasara kwa kukosa ushuru kutoka sekta hiyo muhimu. Hivyo basi, kuokoa sekta ya uchukuzi isiendelee kuyumbishwa na Covid 19 kunafaa kupongezwa.

Baada ya serikali kuonekana kulegeza baadhi ya masharti makali katika sekta mbalimbali, sasa hatua ya kujilinda dhidi ya janga la corona imebakia wajibu wa kila Mkenya.

Hata wale ambao hawatumii usafiri wa umma katika shughuli zao, hawana budi kujilinda kwa maana kwa namna moja au nyingine wataishia kutanganana na wenzao katika shughuli za ujenzi wa taifa.

Mapuuza

Inasikitisha kwamba baadhi ya wananchi siku hizi wameanza kuishi maisha yao kama zamani bila kuzingatia masharti ya kukabili msambao wa corona, yaani wamelegeza kanuni zote kuanzia kunawa mikono, kutumia vieuzi na kuvaa barakoa.

Japo wenye matatu wametakiwa kuzingatia kanuni za kuzuia corona, awali wameonyesha juhudi hafifu mno kuweka mikakati ya kuaminika kukabili maradhi haya.

Kwa hivyo, ili wenye matatu wazingatiwe kuwa kwa kweli wanajali abiria wao na wananchi wote kwa jumla, wanafaa kuweka mikakati ya haraka kuhakikisha hakuna abiria atakayekubaliwa kuingia garini bila kuzingatia kanuni za kuzuia msambao wa Covid 19.

Serikali kupitia wizara ya uchukuzi inafaa kufuatilia jinsi matatu wanavyotekeleza agizo hilo na ikiwa kutakuwa na uvunjaji wa mikakati ya kudhibiti maambukizi ya Covid 19, basi leseni za kuhudumu kwa magari kama hayo zifutiliwe mbali.

Habari zinazohusiana na hii