KINYUA BIN KING’ORI: Polisi wasiegemee mrengo wowote wa kisiasa uchaguzi unaponukia

KINYUA BIN KING’ORI: Polisi wasiegemee mrengo wowote wa kisiasa uchaguzi unaponukia

NA KINYUA BIN KING’ORI

MAAFISA wa usalama huchangia pakubwa kuhakikisha kampeni za uchaguzi zinaendeshwa kwa amani, utulivu, umoja pamoja na na kuwezesha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuandaa uchaguzi huru na wa haki.

Isitoshe, wanahakikisha mazingira ya kupiga kura ni salama bila usumbufu au yeyote kutishiwa maisha.

Ni wajibu wa IEBC kutumia kila mbinu njema kuhakikisha sheria husika zinazingatiwa hata ikimaanisha kushirikisha asasi zingine serikalini kufanikisha uchaguzi ujao.

Polisi ni kiungo muhimu mno kuhakikisha wanasiasa na wafuasi wao wanazingatia kanuni za uchaguzi wakiwa katika kampeni zao. Hata hivyo, maafisa hao wanafaa kuepuka kutumiwa vibaya na viongozi wakuu serikalini kuhangaisha mirengo pinzani kisiasa.

Katiba yetu iko wazi kwamba, ni wajibu wa polisi kulinda usalama wa wananchi wote bila kujali miegemeo ya ya kisiasa,kidini au kijamii.

Polisi kushindwa kulinda maisha ya wananchi kwa sababu ya kupokea maagizo kutoka juu kulichangia raia wengi kupoteza maisha katika uchaguzi mkuu wa 2007. Inaajabisha kwamba, hata kinara wa tume hiyo marehemu Samuel Kivuitu alishindwa kuthibitisha mshindi licha ya aliyekuwa mwaniaji wa Urais wa PNU, marehemu Mwai kibaki kutangazwa mshindi.

Hivyo, polisi na IEBC wakishirikiana ipasavyo, uchaguzi ujao utafanyika kwa njia ya amani bila vurugu zozote.

Polisi wanafaa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kulinda mikutano ya kampeni za wanasiasa wote bila upendeleo. Vile vile, polisi wana nafasi nzuri kuzuia vurugu za uchaguzi kwa kukataa kupokea maagizo yanayoenda kinyume na sheria.

  • Tags

You can share this post!

Daraja la juu ya Thika Superhighway kujengwa Juja

Oparanya akaripia Mudavadi, Weta’ kuhusu maendeleo

T L